SERIKALI imeunda kamati ya watu saba itakayochunguza sakata la matokeo ya mtihani wa uwakili katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Law School), kufuatia kile kinachodaiwa kuwa matokeo mabaya katika mtihani uliofanywa mwaka huu.
Akitangaza kamati hiyo leo Oktoba 12 jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema kamati hiyo itakayoongozwa na aliyekuwa Waziri wa zamani kwa nyakati tofauti na mwanasheria, Dk Harison Mwakyembe imepewa siku 30 za kutoa majibu ya sakata hilo.
Hivi karibuni kumeibuka mjadala kuhusu kile kinachodaiwa kushuka kwa ufaulu wa mawakili katika taasisi hiyo ya uanasheria kwa vitendo, ambapo iliripotiwa kwa taarifa za wanafunzi kuwa na matokeo mabaya.
Illielezwa kuwa katika mtihani uliofanyika mwaka huu, jumla ya wanafunzi 651 katika mtihani huo, 26 pekee wamefaulu, 342 wametakiwa kurudia baadhi ya masomo huku wengine 265 wakiwa wamefeli.