MKUU wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga Mboni Mhita amesema matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ndiyo yatatatua mvutano uliokuwepo wa eneo lipi liweze kuweka mradi wa maendeleo ili kuondoa changamoto kwa wananchi wake.
Mhita alisema hayo jana alipokuwa mgeni rasmi wakati akifungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na Makazi kwa watendaji wa mitaa, kata na makundi mbalimbali katika Manispaa ya Kahama.
Mhita alisema takwimu ndiyo msingi wa kufanya maendeleo kwa wananchi kwani hivi Sasa takwimu zimekuja kutatua mvutano wa migogoro uliokuwepo wa wapi iwe Zahanati,shule au bweni kwaajili ya maendeleo na takwimu zitatumika zaidi .
“Matumizi sahihi ya takwimu yatawezesha utumiaji mzuri wa rasilimali za nchi zilizopo na mafunzo haya umuhimu mkubwa ya kuweza kufanya mabadiliko ya kiuchumi”alisema Mhita.
Mhita alisema kwa kuzingatia mahitaji halisi na huduma zinazotolewa viongozi wanatakiwa kuhakikisha mipango ya kuondoa umasikini na kuleta maendeleo yanafanyika kwa kupitia takwimu sanjari na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Mwakilishi wa Mtakwimu mkuu wa Serikali Benedict Mugambi alisema matokeo ya sensa ya watu na Makazi yanatolewa kwa uhitaji wa muhusika ambapo ofisi zao zinaendelea kuchakata Mambo mbalimbali na kuchakata kuanzia ngazi ya Taifa hadi Mitaa na vitongoji.
“Rais ametoa muongozo wa utumiaji wa matokeo ya sensa ya watu na Makazi ambao watu wote tufuate takwimu hatutegemei viongozi ninyi kwenda kinyume na maelekezo haya”alisema Mugambi.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kahama Thomas Myonga alisema kwa Sasa matokeo ya sensa kwa viongozi wa kata na vijiji hawatakwenda kwa kubahatisha kwenye utekelezaji wao kwani watakuwa na uhalisia hata katika utoaji huduma katika Zahanati.
Ofisa kutoka ofisi za takwimu (NBS) DK Mwinyi Omary akisoma kwa kuwasilisha matokeo ya sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022 alisema kwa manispaa ya Kahama ina asilimia 20.
2 ya watu wote waliohesabiwa katika mkoa wa Shinyanga.