BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), limetangaza matokeo ya udahili wa wanafunzi katika kozi mbali mbali za afya na sayansi shirikishi kupitia mfumo wa udahili wa pamoja (CAS) kwa mwaka wa masomo 2023/2024.
Kati ya wanafunzi 24,007 waliowasilisha maombi yao kupitia CAS, waombaji 22,279 walikamilisha maombi yao na kuchaguliwa vyuo na programu walizopenda hata hivyo kati yao 20,234 tu ndio waliopata.
Akizungumza leo Julai 11, 2023 Mkurugenzi wa Udahili , Utahini na Utunuku, Dk Marcelina Baitilwake amesema waombaji 2, 034 hawakuwa na sifa kwenye programu walizoomba.
“Jumla ya waombaji 15, 833 wamechaguliwa kujiunga kwenye vyuo 219 vinavyotoa programu mbali mbali za Afya na Sayansi Shirikishi ambapo wanawake ni 8,248 sawa na asilimia 52 na wanaume ni 7,585 sawa na asilimia 48.”Amesema
Aidha, amesema waombaji 2,868 walichaguliwa kwenye vyuo 48 vya serikali na waombaji 12,965 katika vyuo 171 visivyo vya serikali.
Amesema, waombaji wenye sifa ambao hawakuchaguliwa kutokana na ushindani katika programu na vyuo walivyoomba wanashauriwa kuomba kujiunga katika programu na vyuo vyenye nafasi katika dirisha la awamu ya pili kupitia mfumo wa udahili wa pamoja.
Dk Marcelina amesema, dirisha la awamu ya pili limefunguliwa rasmi leo Julai 11,2023 na litafungwa Agosti 8,2023 na matokeo ya uchaguzi yatatolewa Agosti 13 mwaka huu.
Nae, Meneja wa Utahini na Utunuku Twaha Twaha, akizungumzia sifa za kujiunga na programu za afya na sayansi shirikishi, amesema kuna program 12 ambazo kila program ina sifa zake tofauti, zipo programu ni lazima uwe na ufaulu wa juu wa somo la Kingereza, programu nyingine ni lazima uwe na ufaulu wa juu wa masomo ya Kemia na Fizikia, nyingine ufaulu wa juu wa Baolojia na Fizikia.
“Sifa za kujiunga na udahili wa pamoja zipo 12 na zinapatikana katika kitabu cha mwongozo cha udahili kilichopo kwenye tovuti ya baraza, mtu anayetaka kujiunga na programu yoyote au chuo anatakiwa kutembelea tovuti ya NACTVITE ili aone sifa na programu husika ili ajue program gani itamfaa.”Amesema
Aidha, amesema katika udahili wa pamoja awamu ya kwanza ambao dirisha lilifunguliwa Mei 21 na kufungwa Juni 2023 kuna ambao walifikisha sifa kutokana na programu walizoziomba lakini kutokana na wingi wa watu waliochaguliwa ni 15,000 na wengine hawakuchaguliwa kutokana na ushindani uliokuwepo.
“Lakini pia vyuo vina idadi maalum ya kupokea wanafunzi kutokana na uwezo, mfano Kibaha chenye programu ya ‘Clinical Medicine’ ilikuwa na nafasi 50 lakini wanafunzi ambao walikuwa na sifa ni zaidi ya 2000 katika ushindani huo ni 50 tu ndio walichaguliwa wengine hawakuchaguliwa.
“Hao warudi kwenye mfumo, hawatalipia chochote, na wanaakaunti zao, warudi kwenye mfumo watakuta vyuo ambavyo vina nafasi na programu zao hivyo wataomba huko.”Amesisitiza Twaha.
Pia, amesema changamoto kubwa iliyojitokeza ni baadhi ya vyuo kutuma ujumbe kwa waombaji kuwa wamechaguliwa vyuo fulani kitu ambacho ni kinyume na taratibu hivyo vyuo hivyo wameviathibu.
Hata hivyo, aemsema baadhi ya waombaji hawakukamilisha madai yao kwenye udahili wa pamoja na kwamba wanaendelea kuwafuatilia wale ambao waliweka namba za simu kujua changamoto zipi ziliwakabili na kushindwa kukamilisha maombi yao.
Comments are closed.