MAMBO mbalimbali yalitokea kabla ya kuanza kwa pambano la watani wa jadi la Simba dhidi ya Yanga jana, huku mashabiki wa Msimbazi wakizomea wakionesha kutofurahishwa na kuwemo kwa Erasto Nyoni katika kikosi kilichoanza.
Mashabiki hao walitaka aanze Jonas Mkude au Nassoro Kapama katika nafasi hiyo ya kiungo mzuiaji kwani wengi wakidai kuwa Nyoni sio wa kuanza mchezo kama huo dhidi ya watani wa jadi, ambao kikosi chao kiko moto sana na kinaongoza ligi kwa pointi nyingi.
Awali, saa 5:45 asubuhi, mageti ya Uwanja wa Mkapa yalifunguliwa mapema na mashabiki wachache kuanza kuingia uwanjani.
Licha ya uwepo wa mvua, lakini makundi kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam yalijitokeza na kuanza kuingia uwanjani
Kasi ya mashabiki kuingia uwanjani ilizidi kuongezeka ilipofika saa 7:30 mchana, ambapo magari mengi ya umma yaliyopambwa na rangi nyekundu na nyeupe, na njano na kijani yaliwasili nje ya Uwanja wa Mkapa yakileta mashabiki wa timu hizo mbili.
Mashabiki wengine walikuwa wakiwasili uwanjani hapo na magari yao binafsi na wengine na bodaboda na kufanya umati kuwa mkubwa, huku rangi zinazo tawala zikiwa nyekundu na nyeupe kwa Simba na njano na kijani kwa Yanga
Saa 8:25: Msafara wa basi lililowabeba wachezaji wa Simba liliwasili Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuelekea vyumbani kwa ajili ya kujiandaa kwenda kupasha misuli moto kabla mchezo kuanza.
Dakika tano baadaye saa 8:30, basi lililowabeba wachezaji wa Yanga aina ya Tata Marcopolo nalo liliwasili uwanjani hapo na wachezaji kushuka na kuelekea vyumbani.
Nje ya uwanja mashabiki waliendelea kufurika na kutokea misururu mirefu ya watu waliokuwa wakiingia uwanjani hapo huku askari wa Jeshi la Polisi wakiongeza umakini zaidi.
Hadi sasa 8:45 mchana, uwanja ulizidi kupendeza zaidi baada ya wapenzi wa soka kuendelea kujaa huku wakiwa wamevalia nguo zenye rangi za timu zao.
Saa 9:30 viongozi wa klabu ya Simba wakiongozwa na Murtaza Mangungu na wenzake waliwasili uwanja hapo kwa ajili ya kushuhudia pambano hilo, ambalo Simba ilikuwa na kibarua cha kulipa kisasi baada ya kuonewa katika mechi kadhaa.
Muda mfupi baadae wanaodhaniwa kuwa mashabiki wa Simba walimrusha uwanjani njiwa ambaye akiwa hewani alianza kufukuzwa na kunguru na kusababisha mashabiki wa Yanga kushangilia kwa nguvu.
Saa 10:09: Wachezaji wa Yanga wakiongozwa na Fiston Mayele waliingia uwanjani na kushangiliwa kwa nguvu na mashabiki wao.
Saa 10:11: Wachezaji wa Simba nao waliingia uwanjani na kufanya mazoezi mepesi kwa dakika 22 wakirudi vyumbani saa 10: 36, na dakika mbili baadaye Yanga nao wakafuata kurudi vyumbani.
Saa 10:40: Vikosi vya timu zote mbili vyatajwa na mshereheshaji , huku mashabiki wa Simba wakionesha kutofurahishwa na kikosi chao kilichoanza, ambacho kilikuwa na kipa wa tatu, Ally Salim na beki Erasto Nyoni.