Matumizi holela viuatilifu yasababisha ugumba, saratani

MATUMIZI holela ya viuatilifu katika mazao, mbogamboga na matunda yanasababisha ugumba kwa wanaume, tezi dume wakati kwa wanawake yanasababisha magonjwa ikiwamo saratani ya matiti, imebainika.

Matumizi ya viuatilifu yasiporatibiwa vizuri yanaweza kuingia katika damu kupitia chakula na kuleta madhara makubwa, kwa sumu hiyo kuharibu mfumo wa homoni na kuathiri mfumo wa uzazi wa wanaume kwa kukata mikia ya mbegu za kiume na kusababisha ashindwe kutungisha mimba.

Hali hiyo kwa kiasi fulani imesababisha ndoa nyingi kuvunjika kutokana na kushindwa kupatikana kwa zao la ndoa ambalo ni watoto huku wanawake wakiathirika zaidi kwa kutuhumiwa kuwa ndio chanzo cha tatizo ambalo sio wao waliosababisha, bali lipo kwa mwanaume.

Hayo yamebainika katika utafiti uliohusisha mikoa mitano inayolima na kutumia mbogamboga kwa wingi ambayo ni Dar es Salaam, Iringa, Morogoro, Mbeya, Arusha, Kilimanjaro na Manyara kuhusu usalama wa chakula kutokana na matumizi ya viuatilifu katika mazao ya mbogamboga na matunda.

Aidha, utafiti huo ulibaini kuwa asilimia 47 ya mbogamboga zote zilizochukuliwa sampuli katika masoko mbalimbali zilikutwa na masalia mengi ya viuatilifu na kuashiria kuwa kulikuwa na matumizi yasiyokuwa sahihi ya viuatilifu.

Utafiti huo umebaini mbogamboga zilizochunguzwa za mchicha, sukumawiki, kabichi, karoti, spinachi, majani ya maboga na matembele zinasababisha pia uharibifu wa mfumo wa fahamu wa watoto kuanzia tumboni kwa mama na pia wanapozaliwa na kula mboga zilizo na masalia ya kemikali hizo.

Mtafiti kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu nchini, Dk Jones Kapeleka aliyeongoza utafiti huo uliofanyika mwaka jana, alisema ikiwa wakulima wataacha matumizi holela ya viuatilifu katika mazao ya mbogamboga na matunda, watasaidia kwa kiasi kikubwa kuiepusha jamii na madhara hayo.

Dk Kapeleka aliyasema hayo hivi karibuni wakati alipowasilisha matokeo ya utafiti huo kwa wamiliki wa vyombo vya habari na wahariri katika warsha iliyoandaliwa na Taasisi za Mviwaarusha, IDP na GAIN kuhusu mifumo endelevu ya chakula kuanzia hatua zote za shambani hadi chakula kinafika mezani kuliwa.

Alisema wakulima wanatakiwa kufikiria na kujali afya za watu wengine watakaokula mazao yao kwa kuwa na matumizi salama ya viuatilifu ili kutunza afya za walaji wa mazao kama wanavyojitunza na kujilinda wakati wakinyunyiza sumu katika mazao hayo.

“Utafiti uligundua kuwa matumizi ya viuatilifu yameongezeka kwa kiwango cha juu kidogo hali inayosababisha uchafuzi wa chakula kwa maana ya chakula kuwa na masalia ya viuatilifu. Kwa maana hiyo wakulima wasipokuwa na matumizi sahihi ya viuatilifu wanaweza kusababisha madhara kwa afya ya mwanadamu,” alisema Dk Kapeleka.

Alisema juhudi inayofanyika ni kuwaelimisha wakulima namna bora ya kutumia viuatilifu ili kusiwe na masalia katika mazao ya mbogamboga kwa sababu masalia ni matokeo ya matumizi ya viuatilifu yasiyo salama.

Aliongeza kuwa ingawa kwa hali ya sasa kilimo hakiwezi kuendeshwa bila ya matumizi ya viuatilifu, wakulima na wananchi wote wanapaswa kujua kuwa viuatilifu vinatakiwa kutumika katika hali ya usalama zaidi ili kulinda afya za walaji na za kwao wenyewe.

Aliongeza kuwa takwimu za uwepo wa viuatilifu zinaweza kushuka ikiwa wakulima watapewa elimu ya matumizi sahihi ya viuatilifu na aina sahihi ya kiuatilifu wanachotakiwa kutumia katika mazao yake.

Alisema mbali na madhara katika afya ya wananchi, matumizi holela ya viuatilifu yanaharibu soko la nje kwa kuwa mazao yote yanayoenda katika soko la nje yanapimwa katika maabara kujua kama yana masalia ya viuatilifu kwa ajili ya kulinda afya za walaji wa nje.

“Tafiti zimeonesha kuwa hata vyakula vilivyopikwa kupitia sampuli zilizochukuliwa na kupelekwa katika maabara vilikutwa kuwa na masalia ya kemikali za sumu kutokana na viuatilifu vilivyotumika kiholela na kutoa uhakika kuwa hata katika vyakula tunavyokula vinakuwa na sumu kwa kuwa kulikuwa na matumizi makubwa ya viuatilifu,” aliongeza.

 

Habari Zifananazo

Back to top button