USUGU wa vimelea dhidi ya dawa ni janga linaloikabili dunia kwa sasa. Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani, kwa kiasi kikubwa inakabiliwa na janga hili la usugu wa vimelea dhidi ya dawa.
Changamoto hiyo inatajwa kuongezeka na kugharimu afya ya umma na uchumi duniani, kwani inatambuliwa kama janga ambalo linatishia na kugharimu idadi kubwa ya maisha ya binadamu.
Inakadiriwa kuwa kama hatua madhubuti hazitachukuliwa janga hili litaua watu milioni 10 kwa mwaka ifikapo 2050 kwani tathmini iliyofanywa mwaka 2019 ilionesha uwepo na vifo vya watu takribani milioni 1.27, ambavyo vilisababishwa moja kwa moja na vimelea sugu kwa dawa.
Idadi ya vifo hivyo vinatajwa kuwa vingi ikilinganishwa na watu waliokufa kwa Virusi vya Ukimwi (VVU) au malaria.
VISABABISHI
Usugu wa vimelea dhidi ya dawa husababishwa na matumizi holela ya dawa dhidi ya vimelea kwa binadamu na kwa wanyama bila ushauri wa wataalamu wa afya, kutumia dawa bila kufanya uchunguzi wa vipimo vya maabara ili kujua dawa sahihi, kutokumaliza dozi kutokana na maelekezo ya wataalamu wa afya.
Twakwimu zinaonesha matumizi ya dawa dhidi ya vimelea nchini yanakadiriwa kufikia asilimia 62.3 na makadirio ya usugu katika sekta ya afya ya binadamu ni asilimia 59.8.
Makadirio hayo yanadhaniwa kuwa makubwa zaidi katika sekta ya mifugo na uvuvi ambapo tafiti zinaonesha asilimia 90 ya wafugaji wanatumia dawa dhidi ya vimelea kutibu wanyama badala ya chanjo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Mecky Matee anasema amefanya utafiti wa usugu wa vimelea vya dawa kwa magonjwa ya kuambukiza yanayotibiwa kwa dawa za antibiotiki.
Anasema vimelea ambavyo vinaoteshwa na wagonjwa ni asilimia 30 hadi 60 ambavyo vinaweza kuwa na usugu wa dawa.
Profesa Matee anasema vimelea sugu vinapatikana katika kila idara ikiwemo kwa binadamu, wanyama na mazingira.
Pia anasema matumizi mabaya ya dawa yanafanyika nchi nzima kwa watu kununua dawa famasi bila kuwa na vyeti, kutomaliza dozi na kuuzwa kwa dawa bila kuwa na mwisho wa matumizi.
Anasema asilimia 30 ya dawa zinazouzwa kwenye famasi, ubora wake unatia shaka kwani hazina mwisho wa matumizi wala watengenezaji kitu ambacho husababisha kuchangia usugu wa vimelea hivyo.
Profesa Matee anasema matumizi ya dawa za antibiotiki kwa wanyama ikiwemo ng’ombe, kuku na wengine wanaoliwa huchangia kuenea kwa vimelea hivyo.
“Utafiti tuliofanya mwaka jana unaonesha kuwa kuku wanaochinjwa katika masoko ya Dar es Salaam wametumia antibiotiki hususani tetecycline siku chache kabla ya kuchinjwa hivyo mlaji si tu atapata usugu wa dawa bali pia kuchangia matatizo mengine ya afya.
“Mtu akishambuliwa na vimelea hivyo, si rahisi kuvitibu kwa sababu vimejaa kwenye mazingira yetu na kwa wanyama pia hivyo, ili kutatua changamoto hizi sekta zote zishiriki kufanya tafiti ambazo zitaonesha sababu za kuenea kwa vimelea hivi,” anaeleza Profesa Matee.
Anasema ni lazima kuwe na mpango mkakati wa kuwezesha sekta zote ziungane kwani tafiti zinaonesha ushirikiano baina ya wataalamu wa wanyama, binadamu na wanyama pori ni asilimia 10 hadi 15 hivyo lazima juhudi zifanyike.
Pia anasema juhudi nyingine zinazotakiwa ni kuhakikisha wanaelimisha umma juu ya matumizi sahihi ya dawa, kupata ushauri wa daktari na madaktari wafuate ushauri wa wataalamu wa maabara kwani wao ndio wana uwezo wa kujua mgonjwa anakimelea gani na atumie dawa gani kumtibu vinginevyo usugu utaendelea.
UENEAJI VIMELEA
Mkuu wa Idara Microbiolojia na Immunolojia, Dk Agricola Joachim anasema vimelea vya usugu wa dawa vinapatikana katika maeneo mbalimbali ikiwemo samani zilizopo hospitalini au vituo vya afya.
Anasema mgonjwa anaweza kwenda hospitali akiwa na ugonjwa mmoja na kutokana na kutozingatia usafi, hupata usugu ambao husababisha magonjwa mengine.
Dk Joachim anasema mazingira yaliyopo hospitalini hata chini ya sakafu vimelea hivyo vipo, hivyo wagonjwa wasiponawa mikono na maji safi na sabuni hueneza vidudu hivyo.
Vimelea hivi huweza kusababisha magonjwa mbalimbali ikiwemo maambukizi ya nimonia, magonjwa ya tumbo au mchafuko wa damu.
“Unapokwenda kumsalimia mgonjwa hospitalini unaweza kuchukua vimelea vya magonjwa au ukapeleka vimelea kwa sababu ya kutozingatia usafi,” anasema Joachim.
Anasema vimelea vya usugu wa dawa vinaweza kuwepo kwenye vyanzo vya maji endapo hakutakuwa na udhibiti wa vyoo kwa maana ya utiririshaji wa maji taka kwenye mikondo ya maji.
Anasema maji hayo pia hutumika kumwagilia mboga za majani ambazo binadamu hutumia na zinashauriwa zisipikwe sana.
“Tunajichanganya pale tunaposema mboga za majani zisipikwe sana wakati huohuo ukiipika kidogo mlaji anaweza kupata usugu wa dawa. Si vimelea vyote vinaweza kufa wakati wa kuchemsha mboga,” anasema Dk Joachim.
Kwenye maziwa pia, mtu anaweza kunywa yakiwa yamebeba vimelea vya usugu wa dawa kupitia mnyama.
Anasema kuku, nyama, maziwa na mayai pia vinaweza kuwa na vimelea hivyo na kuenea wakati wa kula.
“Wapo wagonjwa ambao wanatakiwa kunywa dawa za siku tano na wanapokwenda kwa famasia huomba nusu dozi na hivyo wanapotumia na kupata nafuu, hawarudi kuchukua dawa nyingine na kusababisha kujenga usugu kwa kila dawa,” anasema Dk Joachim.
Anasema wagonjwa wenye vimelea hivyo hukaa hospitalini muda mrefu na kushindwa kuzalisha mali na kuathiri uchumi wao na wa nchi kwa ujumla.
“Tunahitaji ushirikiano wa kupambana na usugu wa dawa kwa kuhakikisha watu wanatumia dozi kamili..si kila kikohozi au mafua uende kuchukua antibiotiki, tufanye vipimo vya maabara kujua kimelea kilichosababisha ugonjwa na kinatibiwa na dawa ipi, tusitumie dawa kiholela,” anasisitiza.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Muhas, Profesa Erasto Mbugi anasema tafiti wanazofanya zinalenga kutunga sera, kutengeneza miongozo na afua zinazochangia ukuaji wa sekta ya afya nchini.
Anasema lengo la kongamano hilo la 11 ni kukutanisha wadau, watafiti, wanataaluma na wahudumu wa sekta ya afya ili kujadiliana namna bora ya kupambana na usugu wa vimelea vya dawa.
“Utafiti huu katika usugu wa vimelea unalenga kutoa usaidizi kwa mpango wa taifa kupambana na usugu wa vimelea vya dawa kwa binadamu na wanyama,” anasema Profesa Mbugi.
MIKAKATI YA SERIKALI
Serikali ya Tanzania imeendelea kutekeleza mpango kazi wa Taifa wa kupambana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa (National Action plan on antimicrobial resistance (NAP –AMR, 2023-2028) katika mfumo shirikishi wa Afya Moja ‘One- Health approach’.
Mpango kazi huo umeainisha afua mbalimbali na malengo ya kimkakati kupunguza kasi ya usugu ambayo ni kuelimisha na kujenga uelewa wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa, utafiti na ufuatiliaji, uzuiaji wa maambukizi ya vimelea vya magonjwa, matumizi sahihi ya dawa, haswa zinazonuia kupambana na vimelea, na uwekezaji endelevu katika mapambano ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu anasema tafiti katika eneo hilo ni muhimu kwani zinatoa taswira sahihi na kushauri njia bora za kuzuia au kupambana na janga hili.
Anasema wanatoa mafunzo na kuzijengea uwezo maabara za afya ya binadamu na wanyama kukabiliana na tatizo hilo.
Profesa Nagu anasema wananchi wanapaswa kutumia wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kutumia dawa dhidi ya vimelea kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya na vipimo vya maabara.
“Kwenye vituo vya afya tutumie maabara zetu kujua maambukizi kwa wagonjwa kabla ya kutoa dawa dhidi ya vimelea. Hii itazuia matumizi holela na hivyo kupunguza usugu dhidi ya dawa,” anasema Profesa Nagu.