Matumizi holela ya dawa yanavyoua kimyakimya

Matumizi holela ya dawa yanavyoua kimyakimya

USUGU wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa za anatibiotiki ni tatizo linalotokana na watumiaji kutokuzingatia matumizi sahihi kama inavyoelekezwa na wataalmu.

Matumizi yasiyo sahihi ya dawa yanajumuisha kutokumaliza dozi kamili iliyopangwa pamoja na kutumia dawa bila ushauri wa mtaalamu wa afya kwa nia tofautitofauti.

Tatizo hilo husababisha dawa mbalimbali ambazo awali zilikuwa zikitibu magonjwa kwa binadamu na kwa wanyama mbalimbali, sasa kutofanya kazi.

Advertisement

Kwa mujibu wa wataalamu, hii inasababishwa na vimelewa vya magonjwa kujibadilisha viini tete vyake au DNA, na kujijengea hali ya kujikinga dhidi ya mazingira mbalimbali. Kwa kufanya hivyo wanasema, vimelea hivyo hukabiliana na ukali wa dawa inapotumika kutibu.

Sababu nyingine ni watu kula mazao ya mifugo au ya kilimo kutoka katika maeneo yaliyotumia dawa mara kwa mara hata kwa kiwango kidogo. Mfano, mifugo kama mbuzi au kuku wakipewa dawa kutibu ugonjwa, kunakuwa na kipindi cha mpito.

Katika kipindi hicho, mazao ya mifugo hiyo yanapaswa yasitumike kwa siku tatu, nne au tano kwani binadamu wanapotumia mazao ya mifugo hao, ni hatari kwa vile huwa wanakula dawa hizo kwa dozi kidogokidogo.

Katika mazingira hayo, wanapougua na kwenda hospitali dawa wanazopewa, hushindwa kutibu maradhi kwani zimeshakuwa sugu mwilini. Hali huwa hivyo hivyo hata katika mimea.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, mimea nayo inaweza kupuliziwa dawa dhidi ya wadudu waharibifu shambani. Kwamba, ni hatari mtu anapopuliza dawa asubuhi katika bustani ya nyanya au mbogamboga, jioni akachuma na kupeleka sokoni au nyumbani kutumia.

Wanasema kwa kufanya hivyo, walaji wanakula hata zile kemikali zilizoko kwenye mazao.

HALI ILIVYO

Mzigo utokanao na usugu wa vimelea vya dawa ni tishio duniani. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2019, vifo milioni 4.9 duniani vilihusishwa na maambukizi ya bakteria wenye usugu dhidi ya dawa huku vifo milioni 1.2 vikihusishwa moja kwa moja na usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibiotiki.

WHO inasema vifo hivyo ni vingi kuliko vilivyosababishwa na ukimwi na malaria, Barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, kuna vifo vingi na kwamba, katika kila watu 100,000, watu 99 hufariki dunia.

Kiasi hiki kinazidi makadirio ya vifo 700,000 vya kila mwaka na huenda vitafikia vifo milioni mbili na zaidi ifikapo mwaka 2030.

SERIKALI YATAHADHARISHA

Serikali imetoa tahadhari kuhusu matumizi mabaya ya dawa za antibiotiki. Inasema matumzi holela ya dawa hizo husababisha usugu wa vimelea dhidi ya dawa hali inayoweza kusababisha kupoteza maisha pia.

Akifungua Kongamano la Pili la Afya ya Sayansi Shirikishi kuhusu usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa lililofanyika Dar es Salaam, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu alisema takwimu za tafiti zinaonesha kuwa, matumizi ya dawa za antibiotiki nchini ni asilimia 92 sambamba na usugu wa asilimia 59.8.

Anasema makadirio yanatazamiwa kuwa makubwa katika sekta ya uvivu na mifugo kutokana na utafiti kuonesha asilimia 90 hutumia dawa za antibaiotiki kutibu wanyama badala ya chanjo.

“Leo tuna matukio matatu; kwanza ni kutambulisha Mpango Kazi wa Taifa wa Kupambana na Usugu wa Vimelea Dhidi ya Dawa, pili ni maadhimisho ya Wiki ya Usugu wa Vimelea na tatu, kupokea Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Taifa wa Mapambano wa 2017/2022.

Anasema Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani, inakabiliwa na janga la usugu wa vimelea dhidi ya dawa. Katika mapambano, serikali inatekeleza Mkakati wa 68 wa Kidunia wa Mkutano wa Afya Duniani wa Mwaka 2025.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mpango huo unaainisha afua mbalimbali na malengo matano ya kimkakati katika kupunguza kasi ya usugu. Malengo hayo ni kuelimisha jamii kuhusu usugu, utafiti na uzuiaji, ufatiliaji wa vimelea na magonjwa, matumizi sahihi ya dawa ya antibiotiki na uwekezaji endelevu wa mapambano ya usugu wa vimelea.

“Katika kipindi cha utekelezaji wa mradi huo, tafiti mbalimbali za jamii juu ya uelewa na mtazamo wa vimelea vilifanyika katika mikoa mbalimbali. Utekelezaji wa mpango kazi wa usugu wa dawa umehusisha sekta ya afya, kilimo na mazingira na Wizara ya Afya imekuwa ikiendeshwa kwa kushirikiana,” anasema Profesa Nagu.

Anasema taarifa hiyo imesaidia kuhuisha mitaala ya kufundishia, eneo la ufuatiliaji na wametoa mwongozo wa kufanya utafiti na kufatilia, pamoja na kutoa taarifa.

Profesa Nagu anasema sekta ya afya imefanya maboresho na kuendesha maabara zake katika ugunduzi wa vimelea kupima sampuli mbalimbali kutoka kwa wagonjwa.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau wametoa mafunzo katika maabara ya afya ya binadamu na wanayama. Hadi sasa kuna maabara 25 za afya ya binadamu na 15 za afya za wanyama na hizi zina uwezo mkubwa wa kufanya kazi,” anasema.

MAZAO YASITUMIKE BAADA YA DAWA

Mimea na wanyama pia inaweza kusababisha usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa kutokana na matumizi holela ya dawa ama kutokamilisha dozi ipasavyo. Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Profesa Hezron Nonga, anasema matumizi ya dawa kwa wanyama ni madogo ikilinganishwa na chanjo.

“Tuna dawa ambazo daktari anatoa ushauri na nyingine zinanunuliwa. Matumizi ya dawa za wanyama si makubwa maana pia tunahimiza matumzi zaidi ya chanjo kuliko dawa,” anasema.

Profesa Nonga anasema mwaka 2021/2022 Tanzania imetumia dozi zaidi ya milioni 700 za kuchanja mifugo dhidi ya magonjwa mbalimbali.

“Wizara ya Mifugo tunasisitiza zaidi matumizi ya chanjo na ufugaji bora kwani mnyama hatoweza kuugua na akiugua itaonekana kama ajali,” anasema.

 

Ofisa wa Shirika la Chakula Duniani (FAO) nchini Tanzania, Dk Elibariki Mwakapeje, anasema kama tafiti za WHO zinavyoeleza, hilo ni tatizo linalosababisha madhara makubwa kwa ulimwengu.

Dk Elibariki anasema mifugo na hata kinyesi cha mifugo hao baada ya kutumia dawa hizo, tayari huwa na kiasi kikubwa cha kemikali, Kwa msingi huo anasema, mtu akichukua mbolea hiyo na kuitumia shambani, sumu hiyo itatoka kwenye kinyeshi kwenda kwenye mmea na hadi kwenye mazao.

Anasema wanafanya tafiti kujua mabadiliko ya tabia. Anatoa mfano akisema wanaona maeneo mengi ya wafugaji, wanatumia dawa bila kufuata utaratibu wa kitaalamu.

“Mfugaji mwenyewe anaenda duka la dawa, ananunua na aenda kumdunga au kumtibu myama; na yeye si mtaalamu. Kwa kufanya hivyo, anaweza kutoa kiwango cha dawa ambacho si sahihi kulingana na ugonjwa wenyewe au badala ya dawa za kumeza au maji, anadunga sindano hayo ni matumizi holela ya dawa,” anasisitiza. Anasema ili kuepuka hali hiyo, baada ya kubaini tabia hizo, sasa wanatoa elimu kwa wafugaji kuhusu masuala ya msingi.

“Huwa tunawashauri watoe chanjo kwa mifugo yao ili wasiugue sababu wasipougua hawatalazimika kutumia dawa, lakini pia mifugo ikiugua, wawe na utaratibu wa kutafuta wataalamu wa mifugo,” anasema Dk Elibariki.

Anaongeza: “Wakipewa ushauri wa kitaalamu, wazigatie na dawa itumike kama inavyotakiwa ili tatizo hii liweze kupungua.”

/* */