Matumizi ya akili unde yasififishe uwezo wa waandishi wa habari

HIVI karibuni waandishi wa habari walipewa mafunzo kuhusiana na matumizi ya Akili Unde (AI) na kuhimizwa kuwa makini wakati wanapoandika habari zao ili waweze kutoa taarifa sahihi hasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Mratibu wa Sera na Programu kutoka shirika lisilokuwa la kiserikali la Tech & Media Convergency (TMC), Janeth Kahindi akizungumza katika mafunzo hayo mkoani Dodoma aliwahimiza waandishi wa habari kuwa makini wanapotumia akili unde katika kazi zao ili kuepuka kutoa taarifa au takwimu ambazo sio sahihi.
Ni ukweli usiopingika kwamba kuibuka kwa teknolojia ya akili unde kumeleta mapinduzi makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo taaluma ya uandishi wa habari.
Kwani kwa kutumia akili unde, waandishi wa habari wana uwezo wa kuchakata taarifa kwa haraka, kuandika makala kwa muda mfupi, hata kupata takwimu na uchambuzi kwa urahisi. Hili ni jambo jema, lakini linahitaji tahadhari kubwa.
SOMA: Akili unde isichafue pambazuko la wanawake kuchaguliwa 2025
Ndiyo maana tunaamini mafunzo haya ni mazuri yakitolewa mara kwa mara kwa waandishi kwa sababu ndio uhalisia, kwani hivi sasa teknolojia hiyo imeingia kila sehemu na watu wa kada mbalimbali wanaitumia wakiwemo waandishi wa habari wenyewe.
Tunasema umakini unatakiwa wakati wote na hasa tunasisitiza kipindi hiki kwa sababu tumeshaanza mchakato kuelekea Uchaguzi Mkuu kuanzia kampeni, kupiga kura na hatimaye kutangazwa matokeo.
Sasa kama kalamu za waandishi wa habari hazitatumika vizuri zinaweza kuilinda amani au kuivuruga iwapo watashindwa kuchambua na kuzichakata vizuri taarifa hasa kama watategemea au kutumia akili unde.
Ni kweli matumizi ya teknolojia hii ni makubwa lakini changamoto iliyopo waandishi wanaweza wasipate taarifa sahihi au kupata habari zilizotungwa.
Kwani tofauti na binadamu, akili unde haina dhamira ya kutafuta ukweli, yenyewe kazi yake ni kuchakata taarifa kulingana na data zilizoingizwa na kama zina upungufu au upendeleo, basi matokeo yake ni habari zinazoweza kupotosha jamii.
Kwa maana hiyo ni wajibu wetu kuwakumbusha wanahabari kuwa makini na kukumbuka jukumu lao ni kusimamia ukweli na maadili ya taaluma.
Hivyo matumizi ya akili unde lazima yafanyike kwa uangalifu na kwa kuzingatia misingi ya taaluma ya uandishi wa habari.
Matamanio ya jamii ni kuona waandishi wa habari wanafanya kazi yao kwa weledi na kuepuka kufifisha uwezo wa kutafuta na kuandika habari kwa usahihi.
Bado tunaamini kwamba uwezo wa binadamu wa kuandika habari au taarifa za kijamii, kisiasa ama kiuchumi, ni mkubwa zaidi kuliko wa akili unde.
Hivyo basi, rai yetu kwa waandishi wa habari ni kuendelea kusimamia taaluma, uwezo, ubunifu na vipawa.


