Matunda maboresho ya bandari yaanza kuvunwa

DAR ES SALAAM:MABORESHO ya bandari yaliyofanywa na Serikali nchini yamefanikisha kutua kwa meli kubwa ya utalii ya Norwegian Dawn yenye urefu wa mita 294 katika Bandari ya Dar es salaam ikiwa na watalii 2340 ambao wanakwenda kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii na hivyo kukuza uchumi.

Akizungumza baada ya kupokea meli hiyo Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es salaam, Mrisho Seleiman Mrisho amesema meli hiyo imepokelewa kutoka Bandari ya Mombasa Nchini Kenya baada ya kupitia katika nchi mbalimbali na kwamba kutokana na maboresho hayo Watanzania watarajie kuona meli nyingine kubwa zaidi.

Mkurugenzi wa Huduma za Meli na Uratibu wa shughuli za Bandari Kapteni, Abdulla Mwingamno ambaye amepokea meli hiyo kubwa kwa mara ya kwanza na kuifikisha bandarini amesema miundombinu iliyopo hivi sasa pamoja na wataalamu inakidhi kuingiza meli kubwa zaidi ya hizo jambo ambalo linaleta ushindani wa kidunia.

Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Dk Damas Mfugale amesema watalii hao ni wa kimkakati katika sekta ya utalii nchini na miaka miwili ijayo meli nyingine za aina hiyo zitawasili hivi karibuni hivyo kuendelea kukuza shughuli za uchumi.

Meli hiyo yenye uwezo wa kubeba watu 4700 na baada ya kutoka katika Bandari ya Dar es salaam itakwenda nchini Msumbiji.

Habari Zifananazo

Back to top button