Matunda, mbogamboga zahofiwa usalama

WAKULIMA wa mbogamboga na matunda katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, wanadaiwa kunyunyizia sumu kali za kuua wadudu wakati wa uzalishaji hali inayoweza kuhatarisha afya za walaji.

Diwani wa Viti Maalumu, Kata ya Ikola, Thedy Majaliwa alisema hayo akichangia hoja katika mkutano wa kwanza wa Baraza la Madiwani kwa mwaka wa fedha 2022/2023. Aliomba elimu itolewe kwa wakulima wa mbogamboga na matunda.

“Naomba ikiwezekana mabwana shamba waende kabisa kwenye bustani za wakulima kuwaelimisha jinsi ya kupulizia dawa kwenye zile mbogamboga, yaani wananchi wengi wanalalamika sana hata kama mtu ukiwa na hamu ya kununua mboga ukishika zile mboga zina harufu mbaya kweli ya ile dawa, hamu ya kula mboga inaondoka,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi  Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Shaban Juma aliagiza maofisa kilimo na ugani wote kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa hizo.

Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Tanganyika, Philemon Mwita alisema wamepokea maagizo hayo na watakwenda kutekeleza.

Alishauri wakulima kusubiri muda wa siku saba hadi 14 wakati wa uzalishaji na baada ya kupulizia dawa hizo kabla ya kuzipeleka sokoni ili kuondoa tatizo la kupeleka mboga sokoni zikiwa na mabaki ya dawa.

Habari Zifananazo

Back to top button