Matunda pori haya  ni muhimu mwilini

“UKILA tunda la ntonga moja ni sawa sawa umekula machungwa sita,” hiyo ni kauli ya Martha Ndelemba kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Tumbi mkoani Tabora.

Akizungumza na HabariLEO, Ndelema amesema tunda la ntonga ni miongoni mwa matunda pori mengine yaliyofanyiwa utafiti na kuonekana yanafaa kutengenezea juisi, jam na wine.

Ameyataja matunda hmengine kuwa ni furu, ntalali, mbula,  amla na msasati.

“Hayo matunda yana umuhimu sana katika mwili wa binadamu kwanza ni dawa, pili yana vitamin nyingi sana hasa C, ambapo kwa mfano kama tunda la ntonga kwa utafiti tulioufanya tumeona ukila ntonga moja ni sawa  umekula machungwa sita,” amesema.

Amesema kituo hicho cha Tumbi kinajihusisha na kilimo misitu hivyo teknolojia ya kilimo misitu ni pamoja na utafiti wa miti pori, ambayo ina manufaa kwa jamii.

Amesema japo mkoa huo una miti ya matunda karibu 72 ila Tumbi ilifanya kwa aina hizo sita.

Naye Mtafiti wa kilimo misitu kutoka kituo hicho cha Tumbi, Kassim Masibuka amesema kati ya teknolojia ya kilimo misitu ni pamoja na utafiti wa miti pori ambayo ina manufaa kwa jamii.

“Utafiti wake ulianza kwanza kuyatambua ikaonekana matunda yanafaa kwa tiba lishe kwa sababu yana vitamin na madini mengi lakini yalikuwa yameachwa,” amesema.

Amesema ili kuyaonesha umuhimu wake walianzisha teknolojia za kusindika na kupata bidhaa mbalimbali ambazo ni juisi, jam na mvinyo.

Amesema wamefundisha wakulima na wataalam teknolojia hiyo ya usindikaji nao waweze kufundisha katika ngazi mbalimbali za halmashauri.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk Geofrey Mkamilo amesema jukumu kubwa la taasisi hiyo ni kutafiti, kusimamia, kuhamasisha na kuratibu shughuli za utafiti nchini.

Dk Mkamilo amesema taasisi hiyo imegundua teknolojia mbalimbali ikiwemo aina mbalimbali za mbegu bora lakini pia kuna mbinu za kilimo bora na ubunifu.

Habari Zifananazo

Back to top button