Mauaji yaundiwe mkakati kuyakomesha

UMOJA, amani, upendo na mshikamano ni miongoni mwa sifa ambazo Tanzania imejaliwa kuwa nazo tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1962 kutoka  kwa wakoloni.

Pamoja na sifa hizo, Watanzania pia wanasifika kwa kuwa wakarimu wao kwa wao lakini pia kwa wageni wanaofika nchini kutoka katika mataifa mbalimbali hali inayofanya taifa hili kujizolea sifa mbalimbali.

Hata hivyo mauaji ya mara kwa mara yanayoendelea kujitokeza siku hadi siku hapa nchini, yanapoteza sifa hizo taratibu. Mauaji hayo ni pamoja na yanayotokana na visa vya mahusiano ya mapenzi jambo linalosikitisha hasa kwa nchi kama hii.

Kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu mfululizo, vimeripotiwa vifo vingi kwa wanafamilia kana kwamba tabia hiyo kwa sasa ndiyo kama suluhisho la ndoa na hivyo kuleta dosari katika jamii nzima  hasa kutokana na kujirudia rudia kwa matukio hayo.

Mbali na mauaji ya aina hiyo pia yapo mauaji mengine yanayotokana na ukatili wa kijinsia na mengineyo yote haya ni katika nchi hii inayotajwa kuwa Taifa huru lenye  wananchi waliojawa na upendo baina yao na hata kwa wageni.

Ushauri wangu katika kupunguza au hata kukomesha kabisa matukio haya ni kwa viongozi wetu wa dini kutumia muda wao mwingi kuielimisha na kuitaka jamii kubadilika na kuwa na hofu mbele ya Mungu.

Unapofika mahali unamtoa uhai binadamu mwenzako aliyeumbwa kama wewe, huko ni kumkosea Mungu kwa kuwa hakumuumba .

Viongozi wetu wa dini kama mtasimama katika hili na kulikemea katika nyumba zenu za ibada mnazoziongoza, ni wazi kuwa matendo haya yatapungua au hata kumalizika.

Mwisho ni vyema kila mmoja kwa nafasi yake atambue thamani yake na mwenzie na kuendelea kujenga upendo wa pamoja kila wakati na hata pale unapoona umekosewa basi suluhisho si kumuua kwa kuwa kuna njia nyingi za kutoa suluhu ya jambo hilo.

Wakati mauaji haya yakihitaji mkakati zaidi kutoka kwa wadau tofauti kuyakomesha, kila mtu asimame katika imani zetu za dini na kumuomba Mungu kwa kila tunaloliona kuwa ni gumu. Majibu yake tutayapata kwani tumeambiwa tuombe kwake kwa kila kitu.

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x