SERIKALI imelieleza Bunge kuwa mwaka jana mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda Marekani kupitia mpango wa AGOA yaliongezeka kwa asilimia 126.3.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji amesema Tanzania mwaka jana iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 74.77 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 33.04 kwa mwaka 2021.
Dk Kijaji alisema hayo wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.
“Ongezeko hilo limesababishwa na kuondolewa kwa amri ya kujifungia ndani nchini Marekani kulikotokana na kujilinda na ugonjwa wa Uviko-19.
Bidhaa zilizouzwa kwa wingi katika soko hilo ni nguo na mavazi na bidhaa za mazao ya kilimo,” alisema.
Dk Kijaji aliwaeleza wabunge kuwa kutokana na uwepo wa masoko ya upendeleo bado Tanzania ina fursa ya kuongeza mauzo ya bidhaa hasa bidhaa za kilimo na viwandani lakini kuna changamoto ya uzalishaji mdogo, usio endelevu na masuala ya ubora.
Alisema mwaka jana thamani ya mauzo ya bidhaa kwenda nchi za Bara la Asia hasa nchi za China, India, Japan na Umoja wa Falme za Kiarabu iliongezeka kwa asilimia 64.4 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 4,276.4 kutoka Dola za Marekani milioni 2,601.5 mwaka 2021.
“Bidhaa zilizouzwa kwa wingi ni pamoja na dhahabu, pamba, mbaazi, makaa ya mawe, shaba na tumbaku,” alisema Dk Kijaji.
Alisema mwaka jana thamani ya bidhaa zilizouzwa katika soko la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ilikuwa ni Dola za Marekani milioni 1,802.2.
Dk Kijaji alisema mauzo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 38.2 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 1,303.4 mwaka 2021.
Alisema mwaka jana thamani ya bidhaa za Tanzania zilizouzwa kwenye soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilikuwa Dola za Marekani milioni 1,414.9 ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 1,161.2 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 17.93.
“Hali hiyo ilichangiwa na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa za kilimo, hususani chai, mahindi, ngano, alizeti, mchele, mbogamboga pamoja na bidhaa za viwandani hususani, karatasi, vigae, saruji na chuma.
“Bidhaa zilizouzwa kwa wingi ni pamoja na madini, pamba, chai, parachichi, kahawa, vigae, vyandarua, saruji, sabuni na mafuta ya kupaka,” alisema Dk Kijaji.
Alisema mwaka jana bidhaa zilizoagizwa kutoka soko la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zilikuwa na thamani ya dola za Marekani milioni 551.3 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 653.
9 mwaka 2021, sawa na upungufu wa asilimia 15.7.
Dk Kijaji alisema upungufu huo ulitokana na kuimarika kwa uzalishaji wa bidhaa za viwandani na kuongezeka kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa zilizokuwa zinaagizwa kutoka nchi wanachama zikiwemo juisi mchanganyiko, mabati na bidhaa za chuma.
Alisema mwaka jana thamani ya mauzo ya bidhaa kwenda soko la Ulaya ilipungua hadi Dola za Marekani milioni 955.
6 kutoka Dola za Marekani milioni 1,346.1 mwaka 2021, sawa na upungufu wa asilimia 29.1.
Dk Kijaji alisema kupungua huko kulisababishwa na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19, vita ya Urusi na Ukraine.
Alisema mwaka jana uagizaji wa bidhaa kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU) uliongezeka kwa asilimia 12.4 na kufikia Dola za Marekani milioni 1,720.4 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 1,530.3 mwaka 2021.