Mauzo ya Korosho yatengeneza Sh.Bil 461.8

MTWARA; JUMLA ya tani 208,000 za korosho ghafi zimeuzwa na kuingiza kiasi cha Sh bilioni 461.8  kwa msimu wa 2023/2024.

Korosho hizo ziliuzwa  kwa bei ya chini ya Sh 1,500 na bei ya juu ya Sh 2,190 katika minada 30 ambayo imeshafanyika katika msimu wa 2023/2024.

Taarifa hiyo imetolewa na Bodi ya Korosho Nchini (CBT) katika kikao kazi kilichoandaliwa na bodi hiyo kujadili mwenendo wa mauzo ya korosho ghafi msimu 2023/2024.

“Hadi kufikia tarehe 26/11/2023 jumla ya minada 30 imefanyika na tani 208,232,312 za korosho ghafi zimeuzwa kwenye minada ikilinganishwa na tani 97,930 zilizouzwa katika msimu wa 2022/2023 kwa kipindi kama hiki,” imesema taarifa hiyo.

Akiwasilisha taarifa hiyo katika kikao hicho mjini Mtwara, Mkurungezi wa Masoko  na Udhibiti Ubora wa Bodi hiyo, Revelian Ngaiza amesema uzalishaji msimu huu ni mkubwa ikilinganishwa na mwaka jana.

Amesema hali ya ubora wa korosho zilizouzwa kwenye minada hiyo ni nzuri ambapo Korosho daraja la kwanza ni asilimia 99.83 na daraja la pili ni asilimia 0.17.

Hata hivyo, taarifa hiyo imesema kumejitokeza changamoto kubwa ya kiwango cha unyevu hali ambayo inashusha kiwango cha ubora na bei.

Habari Zifananazo

Back to top button