MAVAZI ni sehemu ya urembo na huvaliwa kulingana na matukio, hafla au shughuli husika. Vilevile mavazi hupendeza zaidi iwapo mvaaji atavaa kulingana na umbo lake.
Ukivaa mavazi kwa mpangilio yatakufanya uonekane nadhifu na mtanashati. Tambua umaridadi huficha umaskini ndio maana jambo muhimu ni kupangilia mavazi yako, sambamba na vikorombwezo vingine kama pochi, viatu, mapambo n.k.
Katika safu yetu leo ya urembo tutaangalia mavazi ya kazini, yatakayokufanya uonekane nadhifu na wa kitajiri.
*Shati/blauzi rangi nyeupe au bluu bahari- rangi hukufanya uonekane nadhifu sana. Jitahidi upate angalau moja. *Suruali rangi nyeusi, bluu iliyokolea/bahari na kijivu. *Sketi ya rangi ya bluu bahari/ iliyokoza, nyeusi au kijivu, jitahidi upate zile nzuri unazoweza kuvaa popote na unazoweza kuvalia shati au blauzi.
*Magauni hapa cheza na mitindo ya gauni kulingana na umbo lako pamoja na urefu ulionao. Inaweza kuwa ni gauni umbo la penseli, za marinda, zenye pemplamu ili zikusaidie pia kuficha kama una katumbo. Lakini pia muhimu kuzingatia rangi.
Kwa kazini inapendekezwa uvae nguo zenye rangi chache kama sio moja. Kama unapendelea rangi nyingi basi kuwa makini na mpangilio wa hizo rangi au maua. *Bleza au koti; makoti yanasaidia sana kunogesha mwonekano. Jitahidi uwe nableza angalau tatu, mfano la rangi nyeusi, bluu, udongo, n.k. Hapa utapata faida ya kurudiarudia nguo zako ili mradi upate bleza zenye rangi nzuri za kutulia. Bleza unaweza kuvaa na gauni, suruali au sketi. *Suti inaweza kuwa ya sketi na blauzi au suruali na koti. Zingatia rangi zilizotulia mfano kijivu, bluu iliyokolea, nyeusi n.k.
Kuwa makini wakati wa kununua suti, hasa ukizingatia suti huwa bei yake ghali kidogo, hivyo nunua ambayo imara na mtindo wake hauishi ili thamani ya fedha yako iendelee kuonekana. Jambo lingine la kuzingatia na mapambo au urembo utakaoendana na mavazi yako kama vile skafu, hereni, viatu vizuri vyeusi au vyenye rangi inayoingiliana na rangi zingine, urefu wa kiatu utaangalia mwenyewe unavyomudu.
Usisahau kubeba mikoba mizuri, beba mkoba wenye ukubwa mzuri kama huna vitu vingi vya kuhifadhi ndani. Zingatia rangi ya mikoba, chagua rangi ya utulivu mfano nyeusi, rangi ya udongo, kahawia, nude n.k.
Zingatia usafi wa mwili wako hasa kinywa na meno, nywele na hakikisha unatoka nadhifu, kama unasuka au unanyoa basi hakikisha unatokea nadhifu. Siku zote kumbuka umaridadi hufunika ufukara, jitahidi uwe na nguo chache nzuri zisizoisha mitindo na imara. Zitunze vizuri , fua kwa maji na sabuni inayotakiwa. Piga pasi usiziache juani kwa muda mrefu. Vilevile unapovaa mapambo au vitu vya ziada hakikisha haviharibu mwonekano wako. Jifunze kupangilia mavazi yako hayo machache kwani yatakuthaminisha kulingana na bajeti yako