Mavunde atangaza ‘neema’ Mlezi

MBUNGE  wa jimbo la Dodoma  Mjini, Anthony Mavunde amekagua na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa madarasa mapya manne na ofisi za walimu katika shule ya Msingi Mlezi na kukagua miundombinu ya Barabara za mtaa wa Mlezi.

Katika ziara hiyo aliyoifanya leo Desemba Mosi, 2022 katika eneo la Mtaa wa Mlezi,Kata ya Hazina, Mavunde ameiagiza kamati ya shule kusimamia kwa ukaribu ujenzi huo ambao unagharimu shilingi milioni 80 ili umalizike kwa wakati na wanafunzi waweze kuyatumia Januari,2023.

Pia, ameahidi kukamilisha ukarabati wa viwanja wa michezo vya mpira wa wavu na miguu kwa kusawazisha uwanja na kuweka magoli ya Chuma.

Aidha, ameahidi pia kurudisha maji katika shule hiyo yaliyokatwa  kutokana na  deni kubwa lililosababishwa na shughuli za ujenzi.

Aidha, kwa  upande wa barabara ambao kazi ya ujenzi wa makaravati na ukarabati wa barabara za Mitaa  ya Kinyambwa na Hazina unaendelea, Mavunde ameahidi kuleta mtambo kutengeneza barabara zote mapema wiki ijayo pamoja na kufungua barabara mpya za mtaa.

Akishukuru kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Hazina Samwel Mziba ameishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kasi kubwa ya ujenzi wa miundombinu ya vyumba vya madarasa na pia ametoa Shukrani kwa Mbunge Mavunde kwa namna ambavyo amekuwa karibu katika kuhudumia wananchi wa kata ya Hazina na mchango mkubwa alioutoa katika kuiendeleza shule ya Msingi Mlezi ikiwemo uwekwaji wa nishati ya umeme katika shule hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button