MBUNGE wa Dodoma mjini, Anthony Mavunde amechangia sh milioni 2 katika kikundi cha Mavunde Garden kilichopo soko la majengo ili kuwaongezea mtaji.
Pia, amekabidhi viti 100 vya mradi wa kikundi,kuwanunulia shamba la ekari 2 kwa ajili ya mbogamboga na matunda,Bima ya Afya kwa ajili ya wanakikundi pamoja na kufunga TV kubwa ndani ya soko ili wafanyabiashara wapate fursa ya kupata habari mbalimbali.

Akizungumza Mavunde amesema, maboresho makubwa ya miundombinu ya masoko ya jijini Dodoma yanayofanywa na serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan yataweka mazingira mazuri ya biashara ya
soko kuu la Majengo ambalo litafanyiwa maboresho makubwa.

Awali, akizungumza Diwani wa Kata ya Majengo Shifaa Ibrahim amemshukuru Mavunde kwa kuwa nguzo kuu ya maendeleo ya soko kuu Majengo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika shughuli za maendeleo katika soko na kata kwa ujumla.
Akishukuru kwa niaba ya Wafanyabiashara, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa soko hilo Godson Rugazama amemshukuru Mavunde kwa namna anavyotoa msaada mkubwa katika kuboresha miundombinu ya soko na kuwawezesha wafanyabiashara kiuchumi kupitia fursa mbalimbali za mikopo hali ambayo imechochea kukua kwa vipato kwa wafanyabiashara hao.