MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde amewapongeza wanachuo wa chuo cha Mipango Dodoma kwa kuwa mstari wa mbele kuchangia damu kwenye benki ya damu salama ili kusaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa damu kwa wakati.
Mavunde, ameyasema katika viwanja vya Chuo cha Mipango Dodoma wakati wa Bonanza la michezo la kuhamasisha uchangiaji damu lililoandaliwa na Bunge la Wanachuo kwa pamoja na serikali ya Wanachuo(MISO).
“Niwapongeze sana kwa utaratibu huu wa kuchangia damu katika benki yetu ya damu,hii ni kuonesha namna ambavyo mnaguswa na matatizo ya wanajamii na ninyi kuwa sehemu ya jamii mmetimiza wajibu wenu.”Amesema
Amesema kumekuwepo na changamoto kubwa ya upatikanaji wa damu pindi inapohitajika kwa wahitaji hasa katika ajali na uzazi.
“Ninyi mmeonesha mfano mzuri wa kuigwa wa kutambua changamoto hizi na kuamua kuchangia damu….; “Nitoe rai kwa vyuo na taasisi nyingine kuona haja ya kutoa mchango wake kwa jamii kama ambavyo imefanywa na wanachuo hawa wa Chuo cha Mipango”Amesema
Awali, akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri alisema ili kukidhi hitaji la damu katika Mkoa huo, lita zaidi ya 4,100 zinahitajika kwa mwaka.
Akishukuru kwa niaba,Mkuu wa Chuo cha Mipango Prof. Hozen Mayaya amewashukuru viongozi hao kutenga muda wa kujumuika na wanachuo katika zoezi la kuchangia damu na kuahidi kuweka utaratibu mzuri kwa kushirikiana na MISO ili zoezi hilo liwe endelevu kila mwaka.
Naye Spika wa Bunge la Wanachuo Jamal Adam amewashukuru wanachuo wote waliojitokeza kuchangia damu na kuwataka jamii hiyo ya wasomi kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto za jamii na kuwa mfano mzuri kwa jamii.