Mawakili 10 kumtetea mjane wa nyama ya swala
CHAMA cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) Kanda ya Iringa kimewataja mawakili 10 kiliowapanga katika maandalizi hadi usikilizwaji wa rufaa ya hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi na 28 ya mwaka 2022 inayomuhusu mjane Maria Emirio Ngoda aliyehukumiwa miaka 22 kwa kosa la kukutwa na vipande 12 vya nyama ya swala.
Hukumu hiyo ilitolewa katika Mahakama ya Mkoa wa Iringa Novemba 3, mwaka huu na Hakimu Mkazi Mkuu Mkoa wa Iringa Said Mkasiwa aliyedai kuridhishwa pasipo shaka kuwa mjane huyo mwenye watoto wanne alikutwa na ndoo iliyokuwa na nyama hiyo yenye thamani ya Sh 900,000.
Akitoa taarifa ya mchakato wa rufaa hiyo ikiwa ni siku moja baada ya TLS kanda hiyo kutangaza kumsaidia mjane huyo kufanya utetezi huo bure, Mwenyekiti wa TLS kanda ya Iringa, Wakili Moses Ambindwile alisema:
“TLS kwa kupitia mawakili hao tayari imepeleka Mahakama Kuu Kanda ya Iringa taarifa ya kukata rufaa na sasa tunasubiri kumbukumbu namba ya mfumo ili taratibu zingine ziendelee.
Mbali na yeye Wakili Ambindwile aliwataja mawakili wengine watakaosimama kumtetea mjane huyo ambaye rufaa ni sehemu ya haki yake kuwa ni pamoja na Dk Rwezaula Kaijage, Frank Ngafumika, Barnabas Nyalusi, Jane Massey, Samson Rutebuka, Joshua Chusi, Innocent Kibadu na Cosmas Kishamawe.
Tangu uhukumu hiyo dhidi ya mjane huyo itolewe na kuripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii kumejitokeza mijadala na hisia tofauti kuhusu maamuzi hayo ya Mahakama.
Baada ya TLS kujitokeza kumsaidia mjane huyo, jana imeripotiwa katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu nia ya Kamati ya Utekelezaji ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kumsaidia mjane huyo kukata rufaa.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda imeonesha kwamba “Pamoja na kwamba maamuzi ya mahakama ni maamuzi ya mahakama” UWT inajitolea kumsaidia mjane huyo katika rufaa yake kwa kuhakikisha anapata uwakilishi wa mawakili wa kutosha.