Mawaziri wakutana kukabili ukatili kijinsia

MAWAZIRI watatu wamekutana kwa ajili ya kujadili jinsi ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia hususani kwa watoto wawapo shuleni na majumbani kutokana na hali hiyo kukua kwa kasi kubwa nchini.
Kikao hicho cha dharura kimewakutanisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima.
Kuhusu kikao hicho cha dharura Waziri Simbachawene alisema kuwa imebidi wakutane kwa kuwa katika sheria na sera zilizopo kuna mambo ambayo yanahitaji kufanyiwa utaratibu wa haraka ili kukabiliana na hali hiyo iliyokithiri kwa kasi katika miaka ya karibuni.
Pia kutokana na unyeti wa jambo hilo, Simbachawene aliagiza makatibu wakuu watatu kutoka wizara hizo kuandaa kikao cha haraka Januari nne mwaka ujao ambacho kitawakutanisha wadau mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na wananchi.
Alisema kwa kipindi cha mwezi mmoja, Rais Samia Suluhu Hassan amezungumzia suala hilo la ukatili wa kijinsia mara saba kwa kuweka msisitizo, hivyo sio jambo la kupuuzia hata kidogo.
Alisema baada ya kikao hicho cha Januari nne, watapeleka ushauri wao na mawazo yao kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili aridhie, aweze kutoa mapendekezo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu juu ya vita hiyo.
Alisema kuhusu suala hilo la ukatili wa watoto shuleni na majumbani, Waziri Gwajima alitamani kama serikali wakutane ili iweze kutoa mapendekezo ya muda mfupi, wa kati na muda mrefu.
Waziri Gwajima alisema suala hilo limefikia hatua ambayo inapaswa liangaliwe zaidi kwa mwaka mpya wa 2023.
Akasema: “Mwaka 2021 walikatiliwa watoto 11,499 ambao bado inaaminika ni asilimia chache ya wale walioripoti. Ulioongoza ni ukatili wa ubakaji, 5,899, waliolawitiwa ni 1,114 na waliopata mimba za utotoni ni 1,677.”
Aliongeza kuwa utafiti unaonesha ukatili huo kwa kiasi kikubwa unafanyika nyumbani walipo baba na mama, ndugu, jamaa na marafiki, asilimia 40 ni nje ya nyumba ikiwemo shuleni.
Kwa upande wake, Profesa Mkenda alisema kuwa shuleni ni sehemu ambayo watoto wanakaa muda mrefu hivyo Wizara ya Elimu ipo tayari kuongeza nguvu kwa kuongeza mwongozo wa kufanya baadhi ya vitu shuleni.
Pia alisema suala la ukatili huo lipo pia kwa vyuo vikuu kwa kuwa nako kuna watoto wengi na pia kuna suala la malazi, hivyo wizara hiyo ipo tayari kuunga mkono jitihada hizo.