Mawaziri watano wajibu hoja ziara ya Chongolo

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo

MAWAZIRI watano wamejibu hoja za Chama Cha Mapinduzi (CCM) alizozitoa Katibu Mkuu wa chama hicho, Daniel Chongolo akiwa katika ziara mkoani Morogoro.

Walijibu hoja hizo katika viwanja vya Sabasaba mjini Morogoro wakati wa sherehe za miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM.

Sherehe hizo zilienda sambamba na kuhitimishwa kwa ziara ya siku tisa ya Chongolo mkoani humo akiwa amefuatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Oganaizesheni, Issa Haji Gavu.

Advertisement

Chongolo alisema katika kuadhimisha miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM sekta zote zilizolalamikiwa mawaziri wanapaswa kujieleza kwa wananchi hatua gani wanachukua kutatua kero hizo kwa sababu serikali ilitoa fedha za kutekeleza majukumu yao.

Mfumuko wa bei

Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe akizungumzia changamoto ya ardhi na mfumuko wa bei alisema mazao ya wakulima si mali ya serikali na serikali imefungua mipaka ili wakulima wauze popote wanapotaka.

“Hatuwezi kumuonea mkulima kwa kuondoa mfumuko wa bei na kumtia umaskini tutakachofanya ni serikali kununua mazao ya wakulima na kuhifadhi na kuyauza kwa bei nafuu kwa wananchi sio wafanyabiashara lakini pia tutapunguza mfumuko wa bei kwa kutoa ruzuku kwa wakulima ili walime zaidi kwa tija na kuvuna mazao mengi na kuyaingiza sokoni,”alisema Bashe.

Kuhusu migogoro ya ardhi ya kilimo alisema skimu za umwagiliaji zitaendelea kujengwa na kuwapanga wakulima ili kulima kwa tija na kuondoa migogoro hiyo.

Mlundikano wa walimu mjini na vifaa tiba

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa kuondoa mlundikano wa walimu mijini na uhaba wa walimu vijijini mkoani Morogoro na maeneo mengine nchini, Naibu Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), David Silinde alisema wamepokea maelekezo na wameanza kuyafanyia kazi.

“Tamisemi tumepokea maelekezo yako na tumeshaanza kuchukua hatua hapa Morogoro, tumehamisha walimu  547 walioko hapa mjini kwenda maeneo ya pembezoni mkoani hapa na tunatumia shilingi  milioni 607 kufanya kazi hii,”alisema Silinde.

Aidha alisema Waziri wa Tamisemi, Angela Kairuki alizionya halmashauri zote ambazo zimepelekewa fedha na hawazitumii ipasavyo na kusababisha kuwepo na kero kwa wananchi.

Silinde pia alisema kila kituo cha afya, zahanati na hospitali  ambazo hazijafungiliwa kutokana  na changamoto ya vifaa tiba na dawa wizara itahakikisha vinapelekwa ili zifungukiwe zitoe huduma kwa wananchi

Kero ya maji

Naibu Waziri wa Maji, Mary Masanja alisema wameanza kutatua kero ya maji kwenye maeneo yasiyo na maji vijijini ambako serikali imetenga shilingi bilioni 72 kushughulikia. Alisema katika hilo Mkoa wa Morogoro umepewa Sh milioni 165 kutatua kero hizo.

Migogoro ya ardhi

Naibu Waziri wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete alisema  vijiji  vyenye migogoro ya ardhi nchini vimebainishwa na kushughulikiwa.

“Mkoani Morogoro tumefanyia maamuzi maeneo yote yenye mgogoro wa ardhi kama Mvomero na Kilombero na tumekagua mashamba 77 na 11 kati yake tumeyafuta na hekta zaidi ya 2,000 zimerudishwa kwa wananchi,”alisema Ridhiwani.

Migogoro ya wafugaji

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema wizara imejipanga kuwahudumia wafugaji kuondokana na ufugaji wa kuhamahama na kuwataka wafuge kisasa.

“Wafugaji wanaotaka kufuga kisasa tuko tayari kuwasaidia kwa kuwapelekea majosho na madume ya kisasa na kuwaunganisha na benki wapate mikopo nafuu,”alisema Ulega.

Alisema wizara imetenga hekta 500 kwa ajili ya wafugaji watoke bonde la mto Kilombero.

Chongolo alisema chama kitaendelea kuisimamia serikali na watendaji ili kuhakikisha ilani ya uchaguzi ya CCM inatekelezwa kama walivyoahidi kwa wananchi hivyo kila kiongozi atimize wajibu wake.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *