Mayanga atamba kuirekebisha Mtibwa

KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga,

KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga, amesema ametumia mapumziko kufanya marekebisho makubwa na katika mchezo wa leo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC leo, lengo ni kupata ushindi.

Mtibwa wanashuka kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Manungu, Turiani, Morogoro baada ya mapumziko ya wiki mbili kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi yanayomalizika leo.

Mtibwa Sugar wanashika nafasi ya nane kwenye msimamo na kujikusanyia pointi 24 wakati wapinzani wao KMC wapo katika nafasi ya tisa wakiwa na pointi 22 baada ya zote kucheza michezo 19.

Advertisement

Akizungumza na HabariLEO, Mayanga alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika, kikosi kiko salama na anaamini wataenda kukutana na upinzani mkubwa kutoka kwa KMC lakini wamejipanga kuondoka na pointi tatu.

“Naamini utakuwa mchezo mgumu, tumetoka kupoteza mchezo uliopita kwenye uwanja wa nyumbani na tayari tumefanyia kazi mapungufu yetu ili tuweze kukusanya pointi tatu.”

“Tunaingia katika mchezo huu tukiwa na lengo la kupata ushindi, tutawaheshimu wapinzani wetu wana timu nzuri na wachezaji wenye ubora hivyo hatuwezi kuwadharau,” alisema Mayanga.

Naye Kocha Mkuu wa KMC, Thiery Hitimana, alisema anaamini utakuwa mchezo mgumu licha ya kuwa wachezaji  wake wako salama na tayari kwa ajili ya kuwakabili Mtibwa Sugar, wanaingia katika mchezo huo wakiwaheshimu wenyeji wao.

“Halina ubishi Mtibwa Sugar wana kikosi bora chenye wachezaji wazuri, lakini tumewaandaa vijana wetu kwa ajili ya mchezo huu, tunawaheshimu na tutaingia katika mchezo huu kutafuta matokeo ya ushindi japokuwa halitakuwa jambo rahisi,” alisema Hitimana.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *