CAIRO, Misri: MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu ya Yanga anayekipiga Pyramids ya nchini Misri, Fiston Mayele ameingia tatu bora ya wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa kiume wa mwaka 2023 kwa wachezaji wanaocheza ndani ya Afrika.
Katika tuzo za shirikisho la soka la Afrika (CAF) zitakazotolewa Desemba 11,2023 nchini Morocco, Mayele atachuana na mshambuliaji Peter Shalulile wa Mamelodi Sundowns na winga Percy Tau wa Al Ahly.
Kocha mkuu wa Simba SC, Adelhak Benchikha pia ameingia ameingia tatu bora ya makocha watatu Afrika wanaowania tuzo ya kocha bora wa mwaka.
Benchikha ameingia katika orodha kutokana na mafaniko aliyopata akiwa na USM Alger ambayo aliiongoza msimu uliopita kushinda Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Yanga na kutwaa CAF Super Cup dhidi ya Al Ahly.
Makocha wengine waliomo katika mbio hizo ni kocha wa timu ya taifa ya Morocco, Walid Regragui na kocha wa Senegal Aliou Cisse.