MSHAMBULIAJI wa Yanga Fiston Mayele na Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda wameng’ara kwenye tuzo za mwezi zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF).
Taarifa ya Idaraha ya Habari ya Bodi ya Ligi Kuu nchini (TPLB), iliyolewa leo, imeeleza kuwa Mayele ameibuka Mchezaji Bora wa mwezi Novemba, huku Mgunda akiibuka Kocha bora wa mwezi huo wa Ligi Kuu ya NBC.
“Kikao cha Kamati ya Tuzo za TFF kilichokutana Dar es Salaam Jumanne Desemba 6, 2022, kilimchagua Mayele, baada ya kuonesha kiwango kizuri kwa mwezi Novemba na kutoa mchango mkubwa kwa Yanga, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao saba, kati ya mabao hayo matatu ‘hat trick’ akifunga katika mchezo mmoja.
“Mayele ambaye pia alihusika na bao moja katika michezo mitano aliyoichezea Yanga mwezi huo, aliwashinda Mosses Phiri wa Simba na Saido Ntibazonkiza wa Geita Gold alioingia nao fainali,”ilisema taarifa hiyo.
Kwa mwezi Novemba Yanga iliifunga Kagera Sugar 0-1, ikaifunga Singida Big Stars mabao 4-1, ikailaza Dodoma Jiji 0-2, pia iliifunga Mbeya City mabao 2-0 na ilipoteza kwa Ihefu mabao 2-1.
“Kwa upande wa Mgunda aliwashinda Hans Pluijm wa Singida Big Stars na Mecky Maxime wa Kagera Sugar, alioingia nao fainali, ambapo kwa mwezi huo Simba iliifunga Ihefu bao 1-0, ikailaza Ruvu Shooting mabao 0-4, iliilaza Polisi Tanzania mabao 1-3, ikatoka sare ya bao 1-1 na timu za Singida Big Stars na Mbeya City,” ilisema taarifa hiyo.
Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Liti uliopo mkoani Singida, Hassan Simba kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Novemba, kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.