Mayeto wampa 5 Rais Samia
Mwandishi WetuJune 11, 2023

WANANCHI wa Mtaa wa Mayeto Hombolo Makulu, jijini Dodoma wamemshukuru Rais Dr Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa ujenzi wa shule ya msingi mpya ya Mayeto.
Shule hiyo itasaidia kupunguza mwendo wa Kilomita 12 walizokuwa wakizitumia kila siku kutembea kwenda katika shule za mitaa ya jirani.

Akizungumza na wananchi wa Mayeto Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo wa ujenzi wa shule na kuwataka wananchi kuitunza na kuiendeleza.
“Mtakumbuka miaka sita iliyopita mimi na ninyi tulichimba msingi na kuanza ujenzi wa shule hii ya Msingi ya Mayeto.
“Ninamshukuru Rais kupitia mradi wa BOOST jumla ya sh milioni 318 zimeletwa hapa kukamilisha ndoto yetu ya miaka mingi sambamba na ujenzi wa sekondari uliokamilika ndani ya eneo hili ambalo limetumia zaidi ya milioni 400
“Ni jukumu letu sasa kuhakikisha tunatunza miundombinu ya shule hii, na pia kusisitiza watoto wetu kutumia nafasi hii kujielimisha ili kuja kuwa msaada kwa jamii yetu.

“Mimi kwa nafasi yangu nitawaunganishia umeme hapa shuleni na pia nitawanunulia Computer kwa ajili ya shughuli za shule.”Amesema Mavunde
Aidha, Diwani wa Kata ya Hombolo Makulu Gideon Nkana akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi ya Mtaa huo wa Mayeto amesema ujenzi wa shule hiyo utasaidia kuwapunguzia mwendo watoto ambao awali walikuwa wanakwenda umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
“Ninataka kuwahakikishia Rais wangu na Mbunge wangu kwamba wananchi wa Mayeto tupo nao bega kwa bega katika kushirikiana nao kuleta maendeleo.”Amesema

Naye Afisa Elimu Msingi Jiji la Dodoma Prisca Myalla amesema ujenzi wa madarasa tisa na matundu ya vyoo 10 chini ya mradi wa BOOST unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni,2023 ili ifikapo Julai 2023 wanafunzi waanze kuyatumia madarasa hayo.