Mazao ya Tanzania yapata soko zuri kimataifa

Mazao ya Tanzania yapata soko zuri kimataifa

SERIKALI imesema mazao kutoka Tanzania, yamekuwa yakiuzwa kwenye soko la  kimataifa, ikiwemo Nchi za Jumuiya ya Ulaya pasipo mashaka yoyote kutokana na kuwa na viwango vinavyokubalika vya ubora, baada ya  Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania(TPHPA), kupata ithibati.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo Antony Mavunde, wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuimarisha huduma za afya za mimea na usalama wa chakula nchini.

“Sasa bidhaa za Tanzania zinauzwa nje ya nchi pasipo mashaka yoyote, baada ya Mamlaka  kupata ithibati , tulipewa kibali kupeleka mazao India, Hispania na Marekani ni hatua kubwa ambayo imefikiwa,Tanzania inatambulika duniani kote,” alisema.

Advertisement

Alisema kuwa mradi huo ni wa  ushirikiano wa ufadhili wa Jumuiya ya Umoja, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO) na Serikali ya Tanzania.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha ukuaji wa sekta ya kilimo, unafikia wastani wa asilimia 10 na mauzo ya mazao ya kilimo yanaongezeka kutoka dola za Marekani Bilioni 1.2 za sasa hadi dola Bilion 5 ifikapo mwaka 2030.

Mwakilishi Mkazi wa Jumuiya ya Ulaya, Cedric Merely alisema kuwa pamoja na mambo mengine mradi huo utanufaisha sekta ya kilimo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao na kuimarisha soko la Kimataifa.

Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani ( FAO), Niyebenyi Tipo, alisema mradi huo umelenga kuhakikisha usalama wa chakula hasa kwa mazao yanayovuka mipaka kwa kuhakikisha yanakuwa na ubora na kuhakikisha usalama wa chakula na FAO watatoa ushirikiano kuhakikisha mradi huo unatekelezeka na unaleta tija.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dk Christine Ishengoma alitaka fedha za mradi zisimamiwe na kufanya kazi iliyokusudiwa.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania, Dk Efrem Njau,  alisema kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kutaijengea mamlaka uwezo katika shughuli zake za kutambua na kubaini visumbufu hatarishi katika mimea na mazao yasafirishwayo kupitia mipaka mbalimbali.