‘Mazingira rafiki huduma za afya yatavutia vijana’

HUDUMA ya afya ya uzazi itawafikia vijana wengi endapo mazingira rafiki kwao yataimarishwa, kwenye zahanati na vituo vya afya.

Hayo yalielezwa jana na daktari bingwa wa magonjwa wa afya ya akili wa Hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili, Fileuka Ngakongwa, wakati  akitoa mafunzo kwa watoa huduma za afya kwa jamii, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

“Vijana wengi hawataki kukaa kwenye foleni kwakuwa wanaogopa, wengine wanahisi aibu kuonekana wakifata huduma za afya ya uzazi, kwa hiyo wakiwekewa mazingira rafiki itawasaida,” alisema Dk Ngokangwa.

Advertisement

Ofisa Miradi wa Jukwaa la Utu wa Mtoto CDF Tarime, Anold Masawe alisema waliwezesha upatikanaji wa mafunzo hayo kwa siku mbili, kwa   wahudumu wa afya katika ngazi za jamii ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduza za afya ya uzazi  kwa vijana.

Ofisa Miradi wa Jukwaa la Utu wa Mtoto CDF Tarime, Anold Masawe akizungumza katika mafunzo hayo. (Picha zote na Editha Majura).

“Mafunzo haya yatawawezesha  kusaidiana na madaktari katika zahanati, vituo vya afya ili kuwapunguzia vijana wanaohitaji huduma za afya ya uzazi changamoto,” alisema  Anold.

Alisema hatua hiyo ilikuja baada ya wao kubaini uwapo wa kundi kubwa la vijana, wanaohitaji huduma hizo, lakini hawajitokezi kwa sababu tofauti, ikiwemo kuhisi aibu ya kuonekana kwenye foleni, wakisubiria kuhudumiwa.

Mhudumu wa afya katika Zahanati ya Nyamara, Paulina Nyamasaga alitaja tatizo jingine linalowakabili vijana wengi kuwa ni  kutokuwa  tayari kupima afya.