Mbarawa: Hakuna atayekosa haki yake
KILIMANJARO: Serikali imesema hakuna mfanyakazi wa iliyokuwa Kampuni ya Uendeshaji na Uendelezaji Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO) atakayekosa haki zake kwa sababu ya shughuli za uendeshaji na usimamizi wa kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro kuhamia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA).
Akizungumza na Menejimenti ya KADCO, TAA na watumishi mkoani Kilimanjaro Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema mabadiliko yote yanayofanywa na Serikali kwenye Taasisi hiyo yamezingatia taratibu zote za kiutumishi ili kuhakikisha kila mtumishi anapata anachostahili kulingana na sheria zilizopo.
“Serikali ilifanya maamuzi ya kuhamisha shughuli za uendeshaji zilizokuwa zinafanywa na KADCO kuhamia TAA na jambo hili limefanywa kwa mapana yake hivyo niwahakikishie watumishi msiwe na shaka wala wasiwasi maslahi yenu yatazingatia katika utekelezaji wa maamuzi yaliyofanywa na serikali’ amesema Waziri Mbarawa.
Waziri Mbarawa amesema ni wakati muafaka kwa TAA kuangalia namna ya kuboresha miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro ili kukiongezea ubora zaidi katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara amesema tayari kazi ya kuangalia maslahi ya watumishi imeanza kufanywa kupitia kamati maalum iliyoundwa katika kipindi hiki cha mpito ili kuhakikisha kila hatua ya utekelezaji inafanyika kwa kuzingatia sheria.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA Mussa Mbura amemuhakikishia Prof. Mbarawa kuwa kila hatua iliyochukuliwa watumishi watashirikishwa ili kuondoa changamoto ambazo zinaweza kujitokeza hasa kwa watumishi ambao wanakaribia kustaafu.
Mwaka 2010 kutokana na uendeshaji usioridhisha wa Kiwanja hicho Serikali iliamua kununua hisa za wanahisa wenza wa KADCO kwa kuvunja mkataba wa wanahisa na hivyo KADCO kumilikiwa na Serikali asilimia 100 ambapo iliendelea kuendesha KIA ikiwa ni Kampuni ya Serikali kupitia Mikataba ya Uendeshaji (Concession Agreement) na Ukodishaji (Lease Agreement) ambayo imefikia ukomo wake Novemba 09, 2023, Serikali imeamua kuhamisha shughuli za Uendeshaji kutoka KADCO kwenda TAA.