Mbaroni kumgeuza mjukuu wa miaka 13 mke, kumpa mimba
MOROGORO; JESHI la Polisi mkoani Morogoro limemtia mbaroni Castro Thomas (55), mkazi wa Lumba chini, Kata ya Kisaki Wilaya ya Morogoro kwa tuhuma ya kumbaka mjukuu wake mwenye umri wa miaka 13 mkazi wa kijiji hicho hadi kumsababishia ujauzito.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema hayo Novemba 3, 2023 , kuwa tukio hilo lilitokea mwishoni mwa Oktoba mwaka huu.
Amesema awali mtoto huyo alikuwa akiishi na baba yake ( jina limehifadhiwa), lakini baadaye alichukuliwa na babu yake huyo mwanzoni mwa mwaka huu 2023, ambapo anatuhumiwa kumgeuza mke kwa kumwingilia kimwili hadi kupata mimba.
“ Kadri siku zilipozidi kwenda ikaja kubainika kwamba mjukuu wake huyo amepata ujauzito unaokaribia kujifungua,” alisema Mkama.
Amesema kutokana na kitendo hicho kiliichukiza jamii na kwa vile walipatiwa elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia walienda kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha polisi, ambaoi upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.