Mbaroni kwa kulevya na kuwaibia wanawake

JESHI la Polisi mkoani Morogoro limekamata watu wawili, Paulo Erick (48) maarufu Shayo na Dickson Mashamu (33) maarufu kwa jina la Tajiri Masu au Papaa.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Fortunatus Musilimu alisema jana kuwa Erick alikuwa akijitambulisha yeye ni daktari katika Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa iliyopo mkoani Dodoma.

Kamanda Musilimu aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, kijana huyo mkazi wa Kihonda Maduka Kumi alikamatwa Septemba 6, mwaka huu majira ya saa saba mchana katika eneo hilo kwenye Manispaa ya Morogoro.

Alisema Erick alikuwa akiendesha magari ya kifahari, aliwapeleka wanawake katika hoteli za kifahari na huko alikuwa akiwapa kitambaa cha kufuta jasho (leso) na walipokitumia kujifuta walipoteza fahamu na aliwaibia simu, fedha na vitu vya thamani.

Kamanda Musilimu alisema Mei 7 mwaka huu alimwibia mwanamke mwenye umri wa miaka 30 mkazi wa Dakawa wilayani Kilombero mkoani humo.

Kwa mujibu wa polisi wizi huo wa Sh 1,450,000, simu mbili aina ya Vivo na nyingine moja aina ya I Phone 7 ulifanyika hotelini mjini Morogoro.

Kamanda Musilimu alisema mtuhumiwa mwingine, Mashamu mkazi wa Buza Tanesco Dar es Salaam alikamatwa Agosti 27 mwaka huu saa 12 jioni eneo la Msamvu wakati akitoka Dar es Salaam.

Alisema mtuhumiwa huyo alimrubuni mwanamke (27) mfanyabiashara mkazi wa Mlandizi mkoani Pwani akamwibia Sh 7,450,000, simu mbili aina ya Nokia ndogo, I phone 8 plus na saa ya mkononi aina ya Rado.

Kamanda Musilimu alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akijifanya ni mtumishi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) makao makuu Dodoma.

Alisema Mashamu alikua akinunua mvinyo red wine au supu na aliweka humo dawa zinazosababisha mtu apoteze fahamu.

Kamanda Musilimu alisema baada ya kuwalewesha alikuwa akiwalazimisha watoe namba za siri za kadi za benki na aliwaibia fedha kwenye akaunti za benki.

Alisema mtuhumiwa hiyo alikuwa akivaa mavazi nadhifu na akiwalenga wanawake wenye uwezo wa kiuchumi na alikuwa akisakwa kwa kufanya matukio kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Arusha yakiwemo ya kulawiti na kubaka wanawake.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button