Mbaroni kwa kutumia fedha za mahindi kununua gari

JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa limemkamata Castory Mapunda (42) anayetuhumiwa kutumia sehemu ya Sh milioni 41 alizopewa kwa ajili ya kununua mahindi tani 60, kujinunulia gari ya kutembelea aina ya Toyota Premier.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi alisema jana kuwa mtuhumiwa huyo mkazi wa Songea mkoani Ruvuma alipewa kiasi hicho cha fedha na Sadiki Kikoti (45) mkazi wa Kibwawa, mjini Iringa.

Kamanda Bukumbi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, mtuhumiwa huyo alifanya wizi huo wa kuaminiwa baada ya kupokea kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti namba yake 0152677424700 ya CRDB benki kutoka kwa mlalamikaji huyo.

“Alitumiwa fedha hizo ili amsaidie Kikoti kununua kiasi hicho cha mahindi. Hata hivyo mtuhumiwa alitoweka na fedha hizo na baada ya kukamatwa na kupekuliwa alikutwa na gari hiyo namba T 269 EAC na alipohijiwa alikiri kuinunua kwa Sh Milioni 18 ambazo ni sehemu ya fedha hizo,” alisema.

Alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika.

Katika tukio lingine, Jeshi hilo limemkamata Alex Peter akiwa na vipande 10 vya meno ya Tembo vyenye thamani ya Sh Milioni 69.9.

Kamanda Bukumbi alisema tukio hilo lilitokea Agosti 25, mwaka huu majira ya saa 11.30 jioni katika eneo la Kinyanambo A kata ya Kinyanambo, mjini Mafinga.

Aidha katika oparesheni yake ya kupambana na uhalifu alisema jeshi lake limemkamata Paulo Kiwale (50) akiwa na silaha mbili aina ya Gobole zilizotengenezwa kienyeji.

Alisema mtuhumiwa huyo, mkazi wa kijiji cha Mkangavila Isimani, Iringa Vijijini alikamatwa Septemba 18, mwaka huu kijijini humo.

“Alipofanyiwa upekuzi, mtuhumiwa huyo alikutwa pia na vifaa anavyotumia kutengeneza silaha hizo ambazo hutumika kwa ajili ya uwindaji haramu,” alisema.

Pamoja na vifaa hivyo, Bukumbi alisema mtuhumiwa huyo atakayefikishwa mahakamani hivikaribuni baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika, alikutwa pia na mafuta ya Simba yaliyohifadhiwa kwenye kopo pamoja na pua mbili za nguruwe pori.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button