Mbaroni kwa mauaji ya mumewe

JESHI la Polisi mkoani hapa linamshikilia Hoka Mazuri na watu wengine wanne wakiwemo wanawake wawili, kwa tuhuma za kula njama na kisha kumuua mume wake kutokana na ugomvi wa kifamilia.

Wengine wanaoshikiliwa kwa mauaji hayo yaliyotekelezwa Desemba Mosi, mwaka huu ni Shija Masalu, Makoye Lusana, Masunga Mange na Paskali Mange.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alisema jana kwamba chanzo cha mauaji hayo ni mume kumfukuza nyumbani kijana wao, Masunga, kwa tuhuma za wizi wa mifugo kijijini kwao Kiliwi.

“Baada ya kumfukuza kijana huyo nyumbani kwa kuepuka aibu ya wanakijiji, mama hakuridhishwa na hatua hiyo, ndipo akapanga njama za mauaji,” alisema Kamanda.

Mama aliwasiliana na Masalu ambaye naye alienda kumtafuta Lusana kwa ajili ya utekelezaji wa mauaji na wakalipwa Sh 800,000 baada ya kukamilisha kazi.

Kwa mujibu wa Kamanda, simu ya kijana wa wanandoa hao, Paskali ndiyo aliyotumia mama kwa mawasiliano ya njama hizo na kijana huyo (Paskali) ndiye aliyelipa fedha baada ya baba yake kuuawa.

Katika tukio jingine, polisi wanamshikilia Mery Seni, mkazi wa Kitangiri wilayani Ilemela kwa tuhuma za kutupa kichanga kinachokadiriwa kuwa na miezi saba.

Kamanda alisema kichanga kiliokotwa Desemba 5, mwaka huu, Mtaa wa Jiwe Kuu na baada ya mahojiano pamoja na uchunguzi wa daktari, binti alithibitika kuwa ndiye aliyefanya kitendo hicho.

“Alikiri na kudai amefanya hivyo kutokana na ugumu wa maisha kwa sababu aliyempa ujauzito alimtelekeza,” alisema na kuongeza kwamba mtuhumiwa atafikishwa mahakamani muda wowote.

Wakati huohuo, polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama limekamata watu ambao idadi yao haikutajwa, kwa tuhuma za wizi wa mali mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya mkoa, ikiwemo mradi wa Daraja la John Pombe Magufuli pamoja na nyavu za uvuvi haramu katika Ziwa Victoria.

Polisi pia imewakamata watuhumiwa 18 kwa kujihusisha na uvunjaji nyumba na maduka na kuiba mali kadhaa ikiwemo pikipiki, redio na televisheni.

Halikadhalika watuhumiwa 104, wanashikiliwa na polisi kwa kujihusisha na dawa za kulevya na pia jeshi hilo limekamata bangi kilogramu 29, gramu 544 na miche 40 ya bangi.

Limekamata pia mirungi kilogramu 62, gramu 620 za pombe aina ya gongo, lita 4,270 za gongo, mitambo 14 ya kutengeneza pombe hiyo na heroin kete tatu.

Habari Zifananazo

Back to top button