Mbeya wazindua wiki nenda kwa usalama

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mbeya, ACP Benjamin Kuzaga amezindua wiki ya nenda kwa usalama barabarani Kimkoa kwa kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto, magari, pikipiki na bajaji.

Akizindua wiki hiyo jana Aprili 12, 2023 katika stendi ya mabasi Kabwe jijini Mbeya, kamanda Kuzaga amewataka madereva wa vyombo vyao vya moto kukaguliwa na wakaguzi wa magari wa Jeshi la Polisi waliopo katika maeneo mbalimbali ya Mbeya.

Amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na kamati ya usalama barabarani na wakuu wa vyuo vya udereva wameandaa mafunzo maalum ya wiki moja kwa madereva wenye leseni lakini hawakupita katika vyuo vya udereva pamoja na wale ambao hawana leseni ili kujifunza na kupata cheti cha uderevakutoka katika chuo kinachotambulika na serikali.

Mwenyekiti wa Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya, Rajab Ghulika amewataka madereva kujitokeza kuhudhuria mafunzo ya udereva ili kuwajengea uwezo na umahiri wa matumizi ya vyombo vya moto ikiwa ni pamoja na kujikumbusha alama na michoro mbalimbali ya usalama barabarani.

Wiki ya nenda kwa usalama barabarani imeambatana na ukaguzi wa vyombo vya moto, ubandikaji stika za nenda kwa usalama, utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara pamoja na utoaji wa mafunzo maalum ya udereva kwa madereva na utoaji vyeti vya udereva kwa wahitimu.

Kilele cha maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kitafanyika Aprili 20, 2023 katika uwanja wa Ruanda Nzovwe Jijini Mbeya.

Habari Zifananazo

Back to top button