Mbinu mpya utafiti zahitajika UDSM

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimesema kwa muda mrefu utafiti umekuwa ukifanyika kwa mbinu za kimazoea sasa umefika wakati wa kutafakari mbinu mpya ili kuondokana na mawazo ya ukoloni, kuja na suluhisho kwa matatizo yanayoibuka.

Rasi wa Ndaki ya Sayansi ya Jamii chuoni hapo, Profesa Christina Noe amesema hayo katika ufunguzi wa warsha ya watafiti iliyofanyika chuoni hapo.

Noe amesema katika kutafakari mbinu hizo mpya, Udsm kimeungana na taasisi za nchi tano za kimataifa, ikiwemo Tanzania Sweden yenye vyuo vikuu vitatu, Mali na Burkina Faso.

“Tunafikiria zaidi namna tunavyofanya utafiti kama inatupa matokeo tunayotaka na inatuwezesha kufikiri kwa namna ya uhuru zaidi ili tuwe na matokeo chanya kwa jamii.

“Kupitia mradi huu, tunataka wanafunzi wetu wawe na mbinu za kufanya utafiti chanya ili kutengeneza kizazi cha kufanya utafiti huru,” amesema.

Kuhusu utafiti kufadhiliwa na mataifa tajiri na hatari ya matokeo yake kuathiriwa na matakwa ya wafadhili, alisema pamoja na kuwategemea wafadhili, lakini matokeo ya utafiti hayaathiriwi na watoa fedha kwani duniani kote vyuo vikuu vikiwemo vya Ulaya hutegemea ufadhili kufanya utafiti.

“Mkakati wetu ni kuhakikisha kule fedha zinazotoka kusitufanye sisi kufanya kila wanachotaka. Sisi tuna maeneo yetu, kuna jamii zetu. Kwa hiyo tunatumia fedha bila ya kulazimishwa kufanya kama wanavyotaka,” amesema.

Kwa upande wake mratibu wa kituo cha jamii na dini chuoni hapo kinachoratibu mradi huo, Thomas Ndaluka amesema lengo lake ni kuona kuwa utafiti unaofanyika unakuwa na uhalisia.

“Tumekuwa utafiti mwingi tu huko nyuma, lakini kwa mradi huu tutakwenda mbele zaidi kwa kuangalia njia zitakazoboresha si tu utafiti bali pia jamii tunazoguswa na utafiti.

Pia tunalenga kubadili fikra za utafiti na jamii zinazoguswa.

“Tunachosema hakuna anayemiliki ujuzi, ni kitu kinachotakiwa kufanywa kwa pamoja. Unapokuwa na wanafunzi wa uzamili, au uzamivu, inabidi kuwa na njia zinazotengeneza ujuzi wa pamoja. Watafiti wanapokwenda kule kijijini tusiende na mawazo kuwa tuna suluhisho la matatizo yao, kwani wale pia wana njia zao za maisha, bali tuwasikilize wanachosema,” amesema.

Naibu Makamu Mkuu chuoni hapo, Profesa Nelson Boniface aliyemwakilisha Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye, amesema ni wajibu wa watafiti kutafuta mbinu mpya za kuondokana na fikra za ukoloni mambo leo na kuangalia uhalisia wa jamii zizilizopo.

Naye Mkuu wa Ushirikiano wa maendeleo wa Ubalozi wa Sweden, Sandra Diesel amesema mwaka huu nchi hiyo inaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano na Tanzania ukiwamo ushirikiano katika utafiti.

Habari Zifananazo

Back to top button