Mbio za Serengeti za hitimishwa Bunda

NAIBU Waziri wa Utalii, Mary Masanja amewataka Wananchi wanaoishi Kanda ya Ziwa kutumia ipasavyo fursa zinazotokana na Serengeti Safari Marathon zinazofanyika kila mwaka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mbio za Serengeti Safari Marathon 2022 katika eneo la Geti Ndabaka Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Waziri Masanja ametaka kila mmoja kuona umuhimu wa kutumia fursa hizo.

Amesema kuwa ni vyema kuandaa mazingira mazuri ya kuvutia watalii wanaokuja nchini hasa kutokana na hamasa iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Filamu ya The Royal Tour.

“Tunatambua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.

Samia Suluhu Hassan amezindua filamu ya Royal Tour lengo ikiwa kuvutia watalii na wawekezaji, hivyo bila ya sisi kuandaa mazingira mazuri hatutaweza kuwapokea vizuri watalii hao,” amesema Masanja.

Aidha, ametoa wito kwa Wakuu wa Wilaya wa Mikoa ya Simiyu, Mara, Geita na Mwanza kuzishirikisha jamii katika kufungua fursa zilizopo Kanda ya Ziwa ikiwa ni pamoja na fursa za uvuvi,mazao ya samaki,mazao ya wanyama wa kufuga,kilimo cha mboga mboga na fursa za uwekezaji

Naibu Waziri Masanja amewaasa waandaaji na washiriki wa mbio hizo kutokata tamaa bali kujenga mshikamano utakaofanikisha ipasavyo mashindano hayo ili kumuunga mkono Rais Samia katika kampeni ya Kutangaza Utalii na uwekezaji kupitia Royal Tour.

Naye, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk Halfan Haule ambaye pia ni Mkuu Wilaya ya Musoma amewataka washiriki wa mbio hizo kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ili kujionea vivutio vilivyoko ndani yake

Kwa upande wake Mwakilishi wa Waandaaji wa Mbio za Serengeti Safari Marathon, Timothy Mdinka amesema mwaka huu mbio hizo zimelenga kuitangaza Royal Tour kwa kuiweka slogan hiyo katika jezi na maonesho ya utalii.

“Mbio hizi za Serengeti Safari Marathon ni za Maendeleo na ni tofauti na marathon za aina yoyote Ile kwa sababu mbio hizi zinatoa fursa ya kukutana wadau wa utalii na kuangalia jinsi gani tutaboresha maisha katika eneo la Serengeti kwa kusimamia msemo wa Serengeti ‘shall never die’

Habari Zifananazo

Back to top button