Mbogwe yazindua chanjo ya surua na rubella

GEITA: Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe imezindua chanjo ya Surua na Rubella ambayo itadumu kwa muda wa siku nne.

Akizungumza katika uzinduzi huo leo Februari 15, 2024 Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Dk Jacob Julius (JaJu) ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo Sakina Mohamed amesema, chanjo ya Surua na Rubella hutolewa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inatolewa kwa mtoto anapotimiza umri wa miezi tisa na awamu ya pili hutolewa kwa mtoto baada ya kutimiza miezi 18.

“Chanjo hii ni salama, serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha inawaokoa watoto dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa kumkinga mtoto tangu akiwa mdogo,” amesema Dk Jacob

Advertisement

Amesema, magonjwa ya Surua na Rubella yanaathiri mfumo wa fahamu na kusababisha madhara kama Upofu, Uziwi na hata kupelekea kifo.

Wilaya ya Mbogwe inatarajia kutoa chanjo hiyo kwa kuwafikia watoto 58,719 hadi kufikia siku ya hitimisho ya zoezi hilo.

Aidha, Jacob amewataka wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi ili lengo lililowekwa na serikali kuweza kutimia kwa kuwafikia watoto wote ndani ya Wilaya hiyo wanaopaswa kupatiwa chanjo hiyo.

Katika hatua nyingine, Dk Jacob, amewaasa wananchi wa Mbogwe kutoa ushirikiano na kuwathamini watoa huduma za afya kwani kazi wanayoifanya ni kubwa na hivyo ni vyema jamii kuwathamini na kuwaombea ili waweze kutoa huduma zao bila kukwazwa.

Pia, amewaasa watumishi wa kada ya afya kutoa huduma kwa kufuata misingi ya viapo vyao na kwa uadilifu na uaminifu ili wananchi wa Mbogwe washuhudie ubora wa huduma lakini pia thamani ya wanaotoa huduma hizo