WILAYA ya Mbulu mkoani Manyara imekamilisha zoezi la kuchagua wachezaji watakaoshiriki mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA).
Hamashauri ya Mji wa Mbulu imeteua wachezaji 89 na walimu10 watakaoshiriki mashindano hayo katika mkoa huo yanayoanza Mei 26, 2023.
Ofisa michezo wa Halmashauri hiyo, Benson Maneno amesema leo kuwa wamefanikiwa kufanya mchujo huo na kupata idadi hiyo ya wachezaji na viongozi 10 watakaoshiriki katika ngazi ya mkoa ili kuunda timu ya mkoa ya Umitashumta.
“Tumejipanga vyema kama Mbulu kuweza kutoa vijana watakaokuwa na uwezo kwenda kuwakilisha mkoa katika michezo ya Umitashumta taifa itakayofanyika mkoani Tabora mapema mwezi Juni,”
Amesema Halmashauri ya Mji wa Mbulu ni mabingwa wa jumla kwa upande wa soka na riadha katika michezo hiyo kwa mkoa huo.
Zoezi la kuchagua wachezaji katika wilaya hiyo lilihusisha wanafunzi 370 kutoka kanda tatu za Nambis, Endagikot na Daudi ambao pamoja walichuana katika viwanja vya CCM Mbulu na hadi mwisho kupatikana kwa wachezaji 89.