Mbunge adai alifukuzwa Chadema bila kujieleza

MBUNGE wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Hawa Mwaifunga ameieleza mahakama kuwa hakuwahi kupewa nafasi ya kujieleza mahali popote kabla Baraza Kuu la Chadema halijapitisha uamuzi wa kuwapigia kura ya kuwafukuza uanachama.

Mwaifunga ambaye ni mpeleka maombi wa 11 katika kesi ya kikatiba aliyofungua na wenzake 18 kupinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022 kuwafukuza uanachama, alieleza hayo jana katika Mahakama Kuu Masjala Kuu wakati wa kusikilizwa kesi hiyo.

Wabunge hao akiwamo Halima Mdee wamefungua shauri dhidi ya Bodi ya Wadhamini iliyosajiliwa ya Chadema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akijibu maswali kutoka kwa mmoja wa mawakili wa wapeleka maombi, Dickson Kilatu kufafanua kuhusu swali la Wakili wa Mjibu Maombi wa kwanza (Bodi ya Wadhamini ya Chadema), Peter Kibatala ya kuwa walipewa nafasi ya kusema chochote kabla ya wajumbe kupiga kura, Mwaifunga alidai nafasi pekee aliyopewa ilikuwa ni kuomba radhi na siyo kusema chochote kwa maana ya kujieleza.

Alieleza kuwa yeye ni mwanachama anayeijua vizuri Katiba ya Chadema, pamoja na sera na mwongozo wake na alijua hilo kabla ya kuwa mwanachama na anajua kuwa mwanachama wa Chadema anapaswa kuijua na kuifuata katiba ya chama.

Aliongeza kuwa Katiba ya Chadema inataka viongozi na wanachama wote kufuata mwongozo wake na pengine katika hilo wangepewa nafasi ya kujieleza.

Mheshimiwa Jaji katika hiyo hakuna kipengele kinachoeleza mwanachama aliyekosea asisikilizwe, lakini inaelekeza mwanachama aliyekosea apewe nafasi ya kujieleza kupitia vikao maalumu,” alidai.

Pia alieleza kuwa hakuridhishwa na kitendo cha wajumbe wa Kamati Kuu kushiriki kupiga kura katika mkutano wa Baraza Kuu kwa kuwa wao ndio waliopitisha uamuzi wa kuwafukuza uanachama awali, uamuzi ambao ndiyo ulizaa mkutano huo wa Baraza Kuu kujadili rufaa yao na baadaye kupigiwa kura za kufukuzwa uanachama.

“Mheshimiwa Jaji, wajumbe wa Kamati Kuu ambao walikuwa 23 walikuwepo kupiga kura, lakini ni wajumbe hao ndiyo walitufukuza kwenye mkutano wa tarehe 27 na haohao walikuwepo kujadili na kufanya uamuzi kwenye mkutano wa Baraza Kuu,” alidai.

“Hivi, isingewezekana hawa watu kukaa pembeni na kuacha wajumbe wa Baraza Kuu wafanye uamuzi bila wao kuwepo? Ni sahihi wao kusikiliza na kufanya uamuzi katika kikao cha Baraza Kuu?” alidai.

Aidha, alidai sababu ya yeye kutamka kwenye kiapo chake kuwa uamuzi wa kufukuzwa kwao umefanywa na Freeman Mbowe na John Mnyika ni kwa kuwa wao ndio viongozi wakuu na barua aliyopokea ya kumfukuza uanachama ilikuwa imesainiwa na Katibu Mkuu wa chama (Mnyika) kwa niaba ya Mwenyekiti (Mbowe).

Katika shauri hilo, wabunge hao pamoja na mambo mengine, wanaiomba mahakama ipitie mchakato na uamuzi huo wa kuwafukuzwa uanachama, kisha itoe amri tatu.

Amri ya kwanza, wanaomba mahakama itengue mchakato na uamuzi wa kuwavua uanachama; mbili iwalazimishe Chadema kuwapa haki ya kuwasikiliza na tatu itoe amri ya zuio dhidi ya Spika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutokuchukua hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapotolewa uamuzi.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x