Mbunge agawa majiko kuokoa misitu Geita

OFISI ya Mbunge wa Jimbo la Geita mjini imegawa jumla ya majiko ya gesi ya kupikia 250 katika vijiji na mitaa 102 iliyopo kwenye kata 13 ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya matumizi ya nishati mbadala.

Majiko hayo yametolewa na ofisi ya Rais Dk Samia Suluhu huku mengine yakinunuliwa na ofisi ya mbunge ambapo wanufaika ni watu wawili kutoka kila kijiji ama mtaa uliopo ndani ya jimbo la Geita mjini.

Mbunge wa wa Geita mjini, Costantine Knayasu amesema hayo katika hafla ya ugawaji wa majiko hayo iliyofanyika katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Geita.

Advertisement

“Lakini pia nimebakiza majiko ambayo nitayagawa kwenye vijiwe 25 vya wauza kahawa wa hapa mjini Geita wakiwemo mama ntilie” Kanyasu amesema na kuongeza;

“Lengo mahususi la mkakati huu ni kupambana na uharibifu wa mazingira, pia kuleta nishati rafiki ambayo inaweza kuhifadhi mazingira lakini pia kulinda afya za kina mama.”

Amesema matumizi ya nishati mbadala itasaidia kupunguza kasi ya uharibifu wa misitu ndani ya wilaya ya Geita ambayo imeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli za ukataji miti hasa kwa kuni na mkaa.

“Nyinyi mnaona Geita ilikuwa na misitu mingi, tulikuwa tunapata mvua mara mbili kwa mwaka mzima, sasa hivi mvua hamna, mvua ikija inakuja nyingi kupita kiasi, kwa sababu tumeharibu sana mazingira.”

Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Merry Mazula amesema hiyo ni hatua kubwa kumkomboa mwanamke kutoka katika athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.

“Tukisema kwa habari ya mabadiliko ya tabia ya nchi, mwathirika wa kwanza ni mwanamke, kwa sababu gani, ukame unapotokea, mtu wa kwanza kupata njaa ni mwanamke na watoto.”

Mmoja ya wanufaika wa majiko hayo, mkazi wa mtaa wa Kiloleli, Salome Philipo amekiri kuwa na furaha kubwa kwa kupata jiko la gesi kwani anajiona sasa ameondokana na utumwa wa kutafuta kuni kila uchwao.

Taarifa ya Ofisi ya Wakala wa Misitu (TFS) wilayani Geita inaonyesha mpaka sasa zaidi ya asilimia 50 ya hifadhi za misitu zimeharibiwa kutokana na uvamizi shughuli za binadamu ikiwemo uchomaji wa mkaa.