MBUNGE wa Vti Maalum kupitia Asasi Zisizo za Kiserikali (NGOs) Neema Lugangira amezindua kampeni yake ya awamu ya pili ya “Pika kwa Gesi, Tunza Mazingira” kwa kushirikiana na Shirika la Agri Thamani na Oryx Tanzania ambapo mitungi 700 imetolewa kwa mama lishe, walimu, viongozi wa dini na mabalozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akikabidhi mitungi hiyo kwa wananchi mkoani Kagera, Lugangira alisema hizo ni jitihada za Rais Samia Suluhu za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia kwa maeneo ya vijijini na mjini .
Alisema Serikali imedhamiria kuhamasisha nishati safi ya kupikia kwa wananchi kuanzia sasa hadi ifikapo mwaka 2032 kila mwananchi wa vijijini na mjini aweze kutumia nishafi safi na rahisi kutumia bila kuathiri mazingira anayoishi.
“Kampeini ya kwanza niliizindua Desemba ambapo niligawa mitungi 300 ya gesi kwa makundi mbalimbali ,na awamu hii yapili nimegawa mitungi 700 kwa makundi mbalimbali akiwemo mama lishe wanaotupikia chakula lengo ni kuhakikisha kila mwananchi anaungana na serikali kutumia nishati safi na kupunguza uchafuzi wa mazingira”. alisema Rugangira
Alitoa wito kwa wananchi na makundi yote ambayo wanaendelea kunufaika na mitungi ya gesi kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri wa serikali na kuwa sehemu ya hamasa ya kuhamasisha nishati hiyo.
Aidha, elimu ya nishati safi na salama ya kupikia pia ilitolewa na Fatma Mwasa, Mkuu wa Mkoa wa Kagera aliyewakilishwa na Erasto Sima, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba kuhusu faida za matumizi ya nishati safi .
Alisema moja ya faida za kupikia nishati safi ni kuendelea kuwa na afya njema, kuokoa muda na gharama za matumizi kwani matumizi ya mkaa na kuni ni gharama kubwa na matumizi ya gesi yanapunguza gharama katika maswala ya mapishi.