Mbunge aipongeza TARURA ujenzi Biharamulo

Mbunge aipongeza TARURA ujenzi Biharamulo

MBUNGE wa Jimbo la Biharamulo, Ezra Chiwelesa amewapongeza wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini  (TARURA), mkoani Kagera, kwa  kutengeneza barabara ya Rukaragata Kibamba kwa kiwango cha lami, jambo ambalo limewezesha wananchi wa Biharamulo kupata huduma nzuri za afya na elimu bila changamoto.

Alisema kuwa katika miaka iliyopita, barabara hiyo ilijaa maji, hali iliyosababisha watoto wengi kukosa haki yao ya elimu,  hasa nyakati za mvua, jambo lililokwamisha kwa muda mrefu wananchi kupata huduma za afya kwa wakati.

“Hapa lazima tuwapongeze TARURA kwa kazi nzuri wanayoifanya, licha ya kuwa wameng’arisha mji wetu kwa barabara za lami, lakini watoto wetu waliokuwa hawawezi kwenda shule nyakati za mvua kwa sasa wanaenda shuleni bila wasiwasi na wanaoenda katika huduma za afya hakuna tatizo la barabara,”alisema Chilewesa”

Advertisement

Aliwahakikishia wananchi wa Wilaya ya Biharamulo kuwa kwa sasa wananchi wategemee mambo makubwa kwenye miundombinu ya barabara, kwa sababu serikali imeongeza bajeti ya Barabara katika wilaya hiyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ngara, Robert Madulu, alisema uwepo wa barabara  hiyo umepunguza maswali kwa wananchi, ambayo yaliulizwa katika kampeni za uchaguzi mwaka  2020.

Alisema wakati wa kampeni hizo, baadhi ya wananchi walihoji kwa nini  barabara za mji wa Biharamulo hazifanani na barabara za miji mingine ya mkoa wa Kagera .

Kwa mujibu wa  Meneja wa TARURA Mkoa wa Kagera, Avith Theodory, mradi wa barabara hiyo umetekelezwa na mkandarasi wa ndani na mkakati wao ni barabara hiyo kukamilika kutoka kilometa moja iliyotengenezwa, hadi kilometa  mbili mwaka huu wa fedha 2022/2023