MBUNGE wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood amekarabati gari la Jeshi la Zimamoto na Ukoaji lililopata hitilafu na kushindwa kutumika kuzima moto umbali wa mita 300 ulioteketeza nyumba na kusababisha kifo cha mtu mmoja mwenye umri wa miaka 80.
Moto huo ulitokea alfajiri ya Julai 11, 2023 katika nyumba iliyopo mtaa wa Kota kata ya SabaSaba Manispaa ya Morogoro.
Abood alifika eneo tukio kuungana na wananchi na kutoa pole kwa familia iliyokumbwa na mkasa wa kuunguliwa kwa nyumba na kupoteza mpendwa wao ikizingatiwa moto huo ulitokea karibu ofisi za mkoa za jeshi hilo takribani mita 200 au 300 kutoka eneo la tukio.
“Bahati mbaya moto uliopoanza huyu mzee wetu alikuwa ndani na hajiwezi , lakini ni mipango ya Mungu,” alisema Abood
“Tunahitaji tuboresha eneo la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ni muhimu kwani hata majuzi nilipata taarifa ya moto umetokea eneo la Kihonda , lakini bahati nzuri nako kwa ushirikiano wa wananchi ikabidi moto huo wazime.” alisema Abood
Mbunge hiyo alisema, moja ya sababu zilizotolewa na Jeshi la Zimamoto na Ukoaji mkoa zinaeleza ya kwamba gari lao lina matatizo .
“Sisi viongozi tupo ni vyema tuweze kuarifiwa kuwa gari lina matatizo na mwenye uwezo anawezakulitengeneza. “ alisema Abood
Mbunge huyo alisema baada ya kuarifiwa ubovu wa gari hilo ,na kuliona alifikia uamuzi kulitengeneza ili liweze kuendelea kutoa huduma kwa wananchi katika matukio ya moto na mafuriko.
“Huduma hii tukiikosa kwa watu wa Morogoro mjini tutakuwa ni watu wa ajabu sana na mimi nikiwa mbunge wa Jimbo la Morogoro sitakubali wananchi wanapata matatizo haya ya kila siku ni moto na hakuna kinacho wasaidia” alisema Abood
Hivyo aliomba apewe orodha ya vifaa vinavyohitajika ili aviagize na kuliwezesha gari hilo litengamae kwa haraka na kufanya kazi ya uokoaji kwa inavyotakiwa.
“Gari hili litarekebishwa ili liweza kupona na kuendelea kufanya kazi zake za kutoa huduma ya majanga ya moto na mafuriko kwani huwezo kujua ni muda gani yatatokea.” alisema Abood.
Abood aliliomba Jeshi hilo kuongeza ubunifu na uharaka kwenye uwajibikaji pindi matukio kama hayo yanapojitokeza ama vinapoonekana viashiria vya ajali hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa akizungumza na wananchi eneo la tukio hilo alisema licha ya baadhi ya vitu kutekekea pia alimtaja mtu mmoja mzee Miti kupoteza maisha.
“Ni mtu mzima aliyejulikana Mzee Miti ambaye alikuwa ni mgonjwa alishindwa kujiokoa kwenye janga hili na amefariki , serikali ya wilaya inatoa pole kwa ndugu na jamaa wa marehemu.” alisema Nsemwa
Mkuu wa Wilaya aliwasihi Wananchi kuwa wangalifu na kuchukua tahadhari wanapopika vyakula hasa wanawake ili kiepusha majanga ya moto.
Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Morogoro, Emmauel Ochieng alisema, gari lao limepatwa na hitirafu na moto ulipotokea iliwalazimu askari kutembea kwa miguu wakibeba vifaa vya kuzima moto na wengine wakitumia usafiri wa bodaboda kufika eneo hilo.
Ochieng alisema kwa Morogoro mjini Jeshi hilo lina mtambo wa kuzimia moto kwa maana ya gari la kuzima moto na kwamba mtambo huo ulipata hitirafu ambapo mtaalamu wa mitambo anaendelea na matengenezo ambayo bado haijategemaa hadi sasa .
“Ilitulazimu askari wa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji kwenda kuzima moto na kutoa ukozi kwa kufika eneo la tukio kwa miguu, askari ametoka kwa miguu hadi eneo la tukio na kuchukua jitihada za makusudi kuweza kuokoa mali na kuzima moto huo” alisema Ochieng
Ochieng alilishukuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Mzinga kwa kuweza kutoa ushirikiano kwa kuwa hali ilikuwa ni mbaya hasa kutokana na miundimbinu ya majengo yaliyojengwa eneo hilo n ani majengo ya zamani.
“Madhara yapo sehemu moto ulipoanzia vitu vimetekelea na kwa masikitiko kuna majeruhi ila kuna mzee wa miaka kama 70 ambaye ni alikuwa ni mgonjwa na hakuweza kutoka mwenyewe kujiokoa“ alisema Ochieng