Mbunge wa Kibiti, Twaha Mpembenwe amesema wananchi wa jimbo lake wanamtaka aruke sarakasi bungeni, Dodoma ili barabara ya Bungu-Nyamisati itengenezwe na kuondokana na adha ya usafiri inayowakabili.
Akichangia hoja katika hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iliyowasilishwa Bungeni Dodoma mapema leo, Jumatano, mbunge huyo amesema Wanachi wake wamemweka kikao juu ya barabara hiyo huku akitakiwa kutumia mbinu mbadala.
“Wananchi wananiuliza (Hivi Mbunge…kuongea unaungea, lakini unashindwa kuruka sarakasi upate barabara hii ya Bungu-Nyamisati? Mbona wenzako wanaruka sarakasi wanapata barabara? Wewe una shida gani?)” amesema Mbunge huyo.
“Mheshimiwa Waziri [Prof Mbarawa] mimi sina uwezo wa kuruka sarakasi…hata haya huyaelewi?,” amehoji huku wabunge wakicheka.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, wazee wa jimbo lake ni wakali hivyo ili kumwondoa na changamoto hizo, Wizara haina budi kutatua kero hiyo.
Mei, mwaka jana, Mbunge wa Mbulu Vijijini (CCM) Flatei Massay aliruka sarakasi bungeni ikiwa ni kuonyesha msisitizo wa hoja yake kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kujenga barabara ya Mbulu hadi Haydom.
Awali Prof Makame Mbarawa alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali inatarajia kutekeleza miradi mipya saba ya barabara pamoja na mingine huku akiliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Wizara yake ya Sh trilioni 2.6.
Barabara zinazotarajiwa kupitia bajeti ijayo ni Ameainisha barabara hizo kuwa ni Kidatu – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Lumecha/Songea (km 435), Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago – Maswa (Simiyu) (km 339) na ile ya Handeni – Kibirashi – Kijungu – Kibaya – Njoro – Olboroti – Mrijochini – Dalai – Chambalo – Chemba – Kwa Mtoro – Singida (km 460).
Nyingine ni barabara ya Arusha – Kibaya – Kongwa Junction (km 453.42), Masasi – Nachingwea – Liwale (km 175), Igawa – Songwe – Tunduma (km 218) pamoja na barabara ya mchepuo ya Uyole – Songwe yenye urefu wa kilometa 48.9 pamoja na Mafinga – Mtwango – Mgololo (km 81).