Mbunge ampa somo Waziri Silaa
DODOMA: Mbunge wa Makunduchi, Haji Amour Haji amemuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, achukulie pongezi anazopewa kama changamoto kuendelea kufanya vizuri zaidi na zisimtoe kwenye reli.
Ametoa kauli hiyo leo Mei 27, 2024, wakati akichangia bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo iliyowasilishwa na Waziri Silaa Mei 24, 2024 jijini Dodoma.
Mbunge huyo amesema jamii inaona namna Waziri Silaa anavyofanya kazi vizuri, hivyo ni busara pongezi zote anazopewa ziwe changamoto kwake kuendelea kufanya kazi na zisimfanye akatoka katika utendaji bora wake.
Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri Silaa alitaja vipaumbele vitano vya wizara hiyo kuwahudumia Watanzania kwa mwaka 2024/2025 na kuliomba Bunge lijadili na kuidhinisha Sh 171,372,508,000, ili kutekeleza majukumu ya wizara hiyo
Waziri Silaa amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi mijini na vijijini, kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi na kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa huduma na upatikanaji wa taarifa za ardhi.
Vipaumble vingine ni kuhakikisha uwepo wa nyumba bora, ukuaji wa sekta ya milki na maendeleo ya makazi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuimarisha mipaka ya kimataifa.