Mbunge aomba wakandarasi wababaishaji wafungiwe
MBUNGE wa Jimbo la Geita mjini, Constantine Kanyasu, ameiomba serikali kuwafungia wakandarasi wanaopewa tenda na kisha kushindwa kutekeleza kazi kadri ya mkataba ili iwe fundisho kwa wengine.
Kanyasu ametoa kauli hiyo alipofanya mahojiano na HabariLeo juu ya kukwama kwa ujenzi wa mita 300 za barabara ya mtaa wa Molinge mjini Geita, baada ya kutelekezwa na mkandarasi.
Kanyasu amesema kwa kuwa wakandarasi wote serikali ina taarifa zao basi ni vyema ikawa inafanyia mapitio kujua utendaji wao na inapobaini mkandarasi mbabaishaji basi afutiwe leseni.
“Hivi tunavyozungumza mkandarasi yule hayupo ‘site’ (eneo la mradi), lakini barabara ile imekuwa ikijaa madimbwi makubwa ya maji na kuleta usumbufu mkubwa kwa wanafunzi na wanajamii.
“Kwa kweli hali ilivyo sasa ni madimbwi makubwa ya maji, yanazuia barabara hiyo kufanya kazi, tunaonekana wazi kwamba tumeshindwa kumsimamia yule mkandarasi,” ameeleza Kanyasu.
“Suluhisho ni kumfutia leseni na kumpa kipindi cha kujiandaa kumlipisha gharama, hatuwezi kuwa na mkandarasi kipindi cha masika amechimba barabara, anajua ni usumbufu, anatoweka ‘site’ miezi mitatu.
“Halafu bado mkandarasi huyo anaendelea na kazi nyingine. Haiwezekani, huyu mtu anatakiwa afutiwe leseni, azuiliwe kufanya kazi sehemu yeyote, yule mhandisi naye afutiwe kibari, au aje atoe maelezo.”
Novemba 30, 2022, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) mkoa wa Geita, Mhandisi Japherson Nnko aliiambia HabariLeo, kuwa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ulitarajiwa kuanza Juni 6, 2022 na kukamilika Novemba 3,2022 kwa gharama ya Sh milioni 230 lakini mkandarasi hajakamilisha.