Mbunge ashangaa CHADEMA kudai “hakikumteua”

MBUNGE wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Cecilia Pareso ameieleza Mahakama kuwa hakuna mtu anayeweza kujiteua mwenyewe kuwa mbunge licha ya chama chake kudai kuwa hakikumteua kushika nafasi hiyo.

Cecilia ambaye ni miongoni wa wambunge 19 wa chama hicho, waliofungua kesi ya kikatiba kupinga kuvuliwa uanachama, aliyasema hayo jana katika Mahakama Kuu Masijala Kuu wakati akijibu maswali ya wakili Peter Kibatala anayewakilisha Chadema, ambaye ni mjibu maombi wa kwanza

Pareso aliyaeleza hayo mbele ya Jaji Cyprian Mkeha anayesikiliza kesi hiyo na alidai kuwa msingi wa kesi yao ni kutosikilizwa mbele ya Baraza Kuu la chama hicho lililofikia uamuzi wa kuwavua uamachama.

Kama ilivyokuwa kwa wabunge wengine waliotanguliwa kuhojiwa, alidai hawakupewa nafasi ya kujieleza mbele ya Baraka Kuu la Chadema siku ya mkutano uliofanyika Mei 11, 2022 kujadili rufaa yao na badala yake walipewa nafasi ya kuomba radhi kabla ya kufikiwa uamuzi wa kupigiwa kura ya kuvuliwa uanachama.

“Licha ya chadema kwa mujibu wa kiapo chao kudai kwamba mpaka leo hawajawahi kuniteua kuwa mbunge wa viti maalumu lakini kwa utaratibu hakuna mtu anayejiteua mwenyewe kuwa mbunge, ingekuwa hivyo kila mtu humu angekuwa mbunge” alidai Cecilia.

Katika hatua nyingine alidai suala la kujadili ubunge wao halikuwa jambo la dharura kwa kuwa walikuwa wameshaapishwa ingawa katiba yao kupitia kamati Kuu Chadema, inaruhusu kushugulikia masuala ya dharua .

“Uteuzi wangu kuwa mbunge haukuwa jambo la dharura,kikao kilihusu mimi kuapishwa kuwa mbunge na wakati wananitumia huo wito tayari nilikuwa nimeshaapishwa hivyo hakukuwa na dharura” aliendelea kudai.

Alikiri kupokea barua ya wito Novemba 25, 2020 kutoka kwa Katibu Mkuu John Mnyika ikimtaka ahudhurie kikao cha Kamati hiyo lakini wakati huo alikuwa Dodoma licha ya kuwa Mnyika alituma wito huo kwa anwani iliyoonesha yeye alikuwa Dar es Salaam.

Katika shauri hilo, wabunge hao pamoja na mambo mengine, waliiomba mahakama hiyo ipitie mchakato na uamuzi huo wa Chadema kuwafukuza uanachama, kisha itoe amri tatu.

Amri ya kwanza, wabunge hao wanaomba mahakama itengue mchakato na uamuzi wa kuwavua uanachama, mbili, iwalazimishe Chadema kuwapa haki ya kuwasikiliza na tatu itoe amri ya zuio dhidi ya Spika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kutokuchukua hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapotolewa uamuzi.

Mei 11, 2022 Baraza Kuu la Chadema lilisikiliza Rufaa ya wabunge hao dhidi ya Kamati Kuu ya Chadema wakipinga uamuzi wa kamati hiyo kuwafukuza uanachama Novemba 27, 2020, uamuzi ambao ulikaziwa na Baraka hilo kwa kuwapigia kura na kura nyingi ziliamua wabunge hao wafukuzwe uanachama.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x