Mbunge asikitishwa kuona shule haina vyoo

MBUNGE wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood amesikitishwa baada ya kubaini kutokuwepo na vyoo vya wanafunzi zaidi 1,000 na  vya walimu wao katika Shule ya Msingi Mgulu wa Ndege, Manispaa ya Morogoro na kulazimika kwenda kujisaidia shule ya jirani Mkundi.

Abood alijionea hali hiyo baada ya kufanya ziara ya kikazi kwenye kata ya Mkundi na kupokelewa diwani wa kata hiyo, Seif Zahoro Chomoka na diwani wa viti maalum, Grace Mkumbae, viongozi wa chama, serikali na wananchi.

Akiwa katika shule hiyo, mbunge hiyo alibaini kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa vyoo, hivyo aliamua kujenga choo cha walimu wa shule hiyo.

Advertisement

Licha ya  kujenga choo  cha walimu pia atachangia kiasi cha Sh milioni 1 zitakaziotumia kulipa fundi atakayejenga vyumba vya madarasa kutokana na  nguvu za wananchi.

Kwa upande wa vyoo vya wanafuzi wa shule hiyo alimuomba Mkurugenzi wa Manispaa kusimamia, licha ya kusema kuwa serikali itajenga vyoo vya  wanafunzi na kazi hiyo itaanza mapema iwezekanavyo.

Mbunge huyo baada ya kujionea miundombinu na usomaji wa wanafunzi aliahidi kutoa kompyuta saba kwa ajili ya wanafunzi na nyingine mbili kwa ajili ya matumizi ya walimu .

Pia ameahidi kuchangia tofali 3,000  na saruji mifuko 50  kwa ajili ya Shule ya Msingi Kilongo Mlimani ama gharama  hiyo ilipie kiwanja iliobaki kama deni la kiwanja cha shule hiyo.

Mbali na huduma za elimu, mbunge huyo alichangia hundi ya Sh milioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mkundi, Manispaa ya Morogoro ambapo ofisi hiyo ujenzi wake umefikia hatua ya madirisha.

Mbunge huyo pia alisikiliza  kero za  wananchi hasa kuhusu  maji, umeme na miundombinu ya barabara ambapo kwa  viongozi husika wa idara ya maji walitoa ahadi kuwa ndani ya wiki nne zijazo wananchi wa kata ya Mkundi watapata maji.

Abood alimshukuru Rais  Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Jimbo la Morogoro Mjini na kuwataka wahusika kutunza miradi hiyo.

Katika hatua nyingine,  Abood amewataka viongozi wa kata hiyo, kufanya tathmini ya bajeti ya kuweka kenchi za jengo la kituo cha polisi Mkundi ili aweze kushughulikia jambo hilo.