MBUNGE wa Jimbo la Kalenga wilayani Iringa, Jackson Kiswaga (CCM) ameahidi kutoa miche ya miti 10,000 kwa wananchi wa jimbo lake ikiwa ni sehemu mikakati yake ya kuhamasisha jamii kulinda rasilimali maji kwa kutunza mazingira pamoja na kupanda miti.
Katika kikao chake alichofanya na viongozi wa Jumuiya ya Wazazi kutoka kata mbalimbali za jimbo hilo, Kiswaga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira aliwatahadharisha watanzania akisema vita ya maji inayanyemelea mataifa mengi duniani.
“Kuna uwezekano kwamba mzozo mkubwa duniani ukawa juu ya maji. Jambo hili ni lazima lirudishwe kwa nguvu kubwa katika mijadala ya umma kwasababu chanzo chake ni uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji, na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo kutokana na uharibifu huo yamesababisha ongezeko la joto na mvua kubwa katika baadhi ya maeneo duniani,” alisema.
Kiswaga alisema utafiti wa mizozo ya maji uliochapishwa na taasisi ya Pacific ya California Marekani imeorodhesha matukio 279 ya migogoro mikubwa ya maji tangu mwaka 2010 katika maeneo mbalimbali duniani jambo linaloashiria uhaba wa rasilimali hiyo muhimu na vita ya kuigombania.
Alisema watafiti wa athari za mazingira wanabashiri kwamba ifikapo mwaka 2050 kutakuwa na wakimbizi wa mazingira watakaokuwa wanatoka eneo moja kwenda eneo lingine ndani na nje ya nchi kufuata maji.
“Kwa bara la Afrika inakadiriwa watu zaidi ya milioni 140 watakuwa wakimbizi wa maji kwasababu ya uharibifu mkubwa wa mazingira katika maeneo yao na hakutakuwa na usalama katika maeneo mapya watakayokwenda,” alisema.
Alisema ni muhimu kwa kila mmoja wetu kitimiza wajibu wake kwani vita hiyo itakapopamba moto athari zake kwa maendeleo na maisha ya watu zitakuwa kubwa kudhibitiwa kirahisi.
Katika kikao hicho na viongozi wa jumuiya hiyo, Kiswaga alitoa pia taarifa ya kazi alizofanya tangu achaguliwe kuwa mbunge wako zilizohusisha zile zinazotokana na utekelezaji wa Ilani ya chama chake, ahadi zake binafsi na wadau wa maendeleo katika jimbo hilo.
Alizungumzia ukuaji wa sekta za kilimo, ufugaji, umeme, maji, afya, barabara, biashara na utalii na matokeo yake kwa maendeleo ya wananchi wa jimbo lake na Taifa kwa ujumla.
Kiswaga amewahamasisha vijana kujikita katika kilimo akisema ni ajira nzuri inayoweza kuwainua kiuchumi kama ikifanywa kwa ufanisi huku akiahidi kuendelea kuiomba serikali itenge ardhi kubwa zaidi kwa ajili ya kundi hilo.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia wenyeviti na makatibu wa wazazi mkoa na wilaya pamoja na katibu wa UWT na Katibu Mwenezi wa wilaya ya Iringa.