Mbunge wa Viti Maalum, Thea Ntara ameitaka Serikali kueleza lini itawasilisha Muswada wa Sheria ya adhabu kali kwa wanaobaka na kulawiti watoto na wanawake.
Amehoji hilo leo, Alhamisi, katika kipindi cha Maswali na Majibu Bungeni, Dodoma, Mbunge huyo amehoji: “Je, ni lini Serikali italeta Muswada wa Sheria ya adhabu kali kwa wanaobaka na kulawiti watoto na wanawake.”
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul inafanya utafiti zaidi ili kuona endapo kuna ulazima wa kufanya maboresho au marekebisho ya Sheria ya makosa ya kujamiana.
Akifafanua zaidi, Gekul amesema Sheria hiyo, Naibu Waziri amesema kwa mujibu wa vifungu 130, 131, 131A na 154 vya Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, ni makosa ya jinai kwa mtu kubaka na kulawiti.
“Makosa yote haya adhabu yake ya juu ni kifungo cha maisha jela, na adhabu ya chini ni kifungo cha miaka 30 jela.
“Aidha kwa makosa yote haya yakitendeka dhidi ya mtoto mwenye umri chini ya miaka 10, adhabu yake ni kifungo cha maisha jela,” ameeleza.
Ameongeza kuwa pamoja na adhabu hizo Mahakama ina mamlaka ya kutoa amri ya ziada ya kumlipa fidia muathirika chini ya kifungu cha 131(1) cha Kanuni za adhabu.