Mbunge ataka ubepari wa serikali madini ya kimkakati

KUTOKANA na umuhimu wa madini ya kimkakati duniani, Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (CCM) ameishauri serikali kufuata mfumo wa ubepari wa serikali (State Capitalism) ambao unatumiwa na mataifa mbalimbali ikiwemo China, India, Brazil na Norway.

Alibainisha hayo wakati akichangia hotuba ya Waziri wa Madini, Doto Biteko, kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 bungeni Dodoma jana.

Profesa Muhongo alisema uchumi unaoongoza duniani nyakati hizi umegawanyika katika aina mbili ikiwemo ubepari wa ubinafsi ambao uko katika nchi za Magharibi na uchumi wa ubepari wa serikali.

Alisema uchumi huo wa ubepari wa serikali umeibuka kwa nguvu; na nchi za China, India, Brazil na Norway zimefanikiwa kwa kutumia aina hiyo ya uchumi.

“Kwa hiyo Sekta ya Madini lazima itupeleke huko, lazima iwepo migodi inayomilikiwa kwa asilimia 100 na serikali, la sivyo hatutatoka, kuanzia mwaka 2023 na kuendelea nadhani kuna haja ya kuchanganya kampuni binafsi lakini za serikali lazima ziwepo,” alisisitiza Profesa Muhongo.

Alisema sekta ya madini kuanzia sasa inapaswa ijihusishe na uwekezaji, maendeleo na ili kufanya hayo, taasisi mbili muhimu zinahitajika ikiwemo Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ili kufanya uchunguzi wa kijiolojia ambao utabainisha aina ya madini yaliyopo na kiasi kilichopo.

Pia alisema wataalamu wengi wa madini wapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma, hivyo maabara za madini katika vyuo hazinabudi kuwezeshwa kwa kuwa hakuna maabara zinazoweza kupima madini hayo mapya ya kimkakati na badala yake kama nchi itaendelea kupokea ripoti kutoka nje ambazo wataalamu wa ndani hawataweza kuzithibitisha.

Aliyataja baadhi ya madini hayo mapya ambayo leseni zake zimeshatolewa kuwa ni PGM (Platinum Group Minerals) ambayo ndani yake kuna aina takribani saba za madini na yote yana thamani.

Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, baadhi ya madini hayo ya kimkakati yanatumika kwenye mashine za XRay na matibabu ya saratani, hivyo kuna haja kwa serikali kuwekeza fedha za kutosha kwenye taasisi za jiolojia na uchunguzi wa kijiolojia.

Habari Zifananazo

Back to top button